Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali la Mheshimiwa, Katani Ahmed Katani, Mbunge wa Tandahimba, kuhusu malipo ya wakulima wa Korosho waliofanya biashara msimu wa mwaka 2017/2018 na iliyokuwa Benki ya Covenant iliyofungwa kabla ya wakulima hawajatoa fedha zao za mauzo ya korosho, bungeni jijini Dodoma.
NA SAIDINA MSANGI NA
FARIDA RAMADHANI, WFM, DODOMA
SERIKALI imesema
imewalipa wakulima wa korosho wilayani Tandahimba mkoani Mtwara zaidi ya
shilingi bilioni 332.7 zikiwa ni bima ya amana kwa wateja wa iliyokuwa Benki ya
Covenant ambayo ilifilisiwa na Serikali kwa mujibu wa sheria.
Hayo
yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad
Hassan Chande (Mb),
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tandahimba Mheshimiwa Katani Ahmed
Katani, aliyetaka kujua ni lini Serikali itawalipa wakulima wa
korosho waliofanya biashara msimu wa mwaka 2017/2018 na iliyokuwa Benki ya
Covenant iliyofungwa kabla ya wakulima hawajatoa fedha zao.
“Hadi kufikia
mwezi Desemba 2021, jumla ya shilingi 332,715,894.00 zimeshalipwa kwa
Wakulima wa Korosho 1,078 kati ya Wakulima 1,346 wa Wilaya ya Tandahimba waliokuwa
na amana katika Benki ya Covenant, ikiwa ni asilimia 98 ya kiasi cha shilingi
337,992,095.00 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia katika kituo cha
Tandahimba,” alisema Mhe. Chande.
Mheshimiwa
Chande alisema kuwa kuanzia mwezi Machi mwaka 2018, Bodi ya Bima ya Amana
ilianza zoezi la kulipa fidia ya bima ya amana ya kiasi kisichozidi shilingi
1,500,000 kwa wateja waliostahili kulipwa bima hiyo wakiwemo wakulima wa
korosho wa Tandahimba na kuwataka wateja ambao hawajachukua fedha zao za bima
wafanye hivyo kwani zoezi la ulipaji bado linaendelea.
Mhe. Chande
alisema kuwa Benki Kuu ya Tanzania iliifutia leseni iliyokuwa Benki ya Covenant
(Covenant Bank for Women (T) Limited) mnamo tarehe 4 Januari 2018 kwa
mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kuteua Bodi ya
Bima ya Amana (Deposit Insurance Board – DIB) kuwa mfilisi wa Benki hiyo.
Alieleza kuwa
Bodi ya Bima ya Amana inaendelea na zoezi la ufilisi wa Benki hiyo kwa
kukusanya mali na madeni ili kupata fedha za kuwalipa wateja waliokuwa na amana
zinazozidi shilingi 1,500,000/= ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu za
ufilisi kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na
kuuza mali za Benki hiyo.
0 Comments