NGOME YA VIJANA ACT-WAZALENDO YAFUNGUKA CHANGAMOTO SITA MIKOPO ELIMU YA JUU


Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa ACT-Wazalendo Abdul Nondo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA ABRAHAM NTAMBARA

NGOME ya Vijana Taifa ACT-Wazalendo imesema kwamba imebaini bado kuna changamoto kadhaa ambazo zinahitaji utatuzi wa Serikali kupitia Bodi ya Mikopo juu ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Akuzungumza na waandishi wa habari leo Juni 5, 2022 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa ACT-Wazalendo Abdul Nondo amesema changamoto hizo wamezichambua katika hoja sita na kutoa mapendekezo ili katika mwaka wa mosomo ujao 2022/2023 zisijirudie tena.

Nondo amezitaja hoja hizo kuwa ni ufinyu wa bajeti katika ugawaji wa mikopo elimu ya juu, ujanja uliotumika katika kufuta tozo/ada ya kutunza thamani ya mkopo (value retention fee/ vrf 6% ) na adhabu ya asilimia 10, Bodi ya Mikopo inaibia wadaiwa/wanufaika wa mikopo elimu ya juu na kuongezwa fedha ya kujikimu kwa wanafunzi kwa siku.

Nyingine ni Benki ya NMB kukopesha wanafunzi wa elimu ya juu kwa riba na hoja ya sita (a) mifumo ya Bodi ya Mikopo inaongezea madeni wadaiwa (b) Serikali ipunguze makato ya asilimia 15 ya kiwango cha marejesho ya mkopo kwa mwezi.

Akizungumzia kuhusu hoja ya ufinyu wa bajeti katika ugawaji wa mikopo hiyo, Nondo amesema ufinyu wa Bajeti katika utoaji wa mikopo elimu ya juu imekuwa changanoto ya muda mrefu ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi walioomba na wenye sifa za kupata mkopo.

“Hata katika taarifa ya CAG ya 2020/2021 ameelezea juu ya wenye sifa kukosa mikopo sababu ya mifumo na uhaba wa fedha /Bajeti. Changamoto hii imejitokeza tena 2021/2022 mbali na kwamba Bajeti ya mkopo elimu ya juu iliongezwa mwaka 2021 kufikia Tsh, Billioni 570 kwa jumla ya wanafunzi 160,000 kati ya hawa wanafunzi wa mwaka wa kwanza ni 62,000 na wanaoendelea au waliopo chuoni ni wanafunzi 98,000,” amesema Nondo na kuongeza,

“Tofauti na mwaka juzi 2020 ambapo ilitolewa Tsh. Bilion 464, mbali na bajeti kuongezwa 2021/2022 bado changamoto ilikuwa kubwa kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi wa mwaka wa kwanza kuomba mkopo, kwani zaidi ya wanafunzi 80,000 wa mwaka wa kwanza waliomba mkopo 2021/2022 na waliopata ni wanafunzi 62,000 wa mwaka wa kwanza,”.

Amebainisha kwamba changamoto hii ilifanya Bodi ya mikopo kugawa fedha kidogo kidogo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza 62,000 hivyo ikapelekea asilimia 75 ya wanufaika kupewa ada Tsh.400,000 kwa mwaka ikiwa ada zao chuoni ni zaidi ya million mbili hadi tatu kwa mwaka.

Kwamba asilimia 90 ya wanufaika wa mkopo walinyimwa kabisa fedha ya vitabu na viandikwa (BS), asilimia 90 ya wanufaika walinyimwa fedha ya mafunzo kwa vitendo na pia asilimia 90 ya wanufaika wanaofanya tafiti walinyimwa fedha ya tafiti.

“Hii iliibua changamoto kubwa sana kwa wanafunzi kwani wapo walioahirisha masomo,wapo walioacha masomo,wapo waliosoma kwa tabu ,wapo ambao changamoto hizi zilishusha uwezo wao katika masomo na wapo ambao hawakufanya mafunzo kwa vitendo kwa ufanisi kwa kukosa fedha,” amesema Nondo.

Hivyo akitoa mapendekezo kwa hoja hiyo, Nondo ameitaka Serikali iongeze fedha ya kutosha katika Bajeti (Sub-vote ) ya Bodi ya mikopo katika mwaka wa fedha unaoingia kwamba tathimini inaonesha, jumla ya wanafunzi 95,955 kidato cha sita mwaka huu wamefanya mtihani na kutarajia kujiunga na chuo pamoja na wanafunzi watakao maliza stashahada (Diploma).

Kwamba tathimini inaonesha mwaka huu 2022/2023 zaidi ya wanafunzi laki moja wa mwaka wa kwanza tuu wataomba mkopo, tofauti na mwaka jana 2021/2022 ambapo zaidi ya wanafunzi 80,000 wa mwaka wa kwanza ndiyo walioomba mkopo.

Vile vile ameitaka Bodi ya mikopo igawe mikopo kwa wanafunzi kwa lengo la kusaidia wanafunzi kuumudu gharama za masomo kulingana na mgawanyo unaotakiwa ambapo ameeleza kuwa Bodi ya mikopo imekuwa ikigawa mikopo kwa kiwango cha chini kabisa bila kujali mzigo ambao mwanafunzi anabaki nao juu ya gharama ambazo anatakiwa yeye kulipa,mfano.

“Mwaka jana 2021/2022 Wanafunzi walionufaika asilimia 75 walipewa ada Tsh.400,000 ikiwa ada za vyuo ni zaidi ya million mbili, asilimia 90 ya wanufaika wa mkopo walinyimwa kabisa fedha ya vitabu na viandikwa (BS) waliyopaswa kupewa Tsh.200,000 kwa mwaka, asilimia 90 ya wanufaika walinyimwa fedha ya mafunzo kwa vitendo waliopaswa kupewa Tsh.560,000 kwa siku 56 wawapo kwenye mafunzo kwa vitendo na asilimia 90 ya wanufaika wanaofanya tafiti walinyimwa fedha ya tafiti. Makosa haya hayapaswi kurudiwa katika mwaka ujao wa masomo 2022/2023,” amesema Nondo.

 

Post a Comment

0 Comments