Na Mwandishi wetu, Tanga.
Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wameishauri Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) kuendelea kubuni mazao mapya ya utalii katika mapango ya Amboni yaliyopo mkoani Tanga ili kutoa fursa kwa wageni wengi zaidi kutembelea kivutio hicho ambacho ni urithi wa mambo kale.
Akitoa maelekezo ya kamati hiyo kwa wizara ya Maliasili na Utalii mara baada ya ziara ya kikazi katika mapango hayo mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii mheshimiwa Timotheo Mnzava amesema kuwa eneo hilo lina fursa nyingi la mazao mapya ya utalii hivyo ni jukumu la wizara na NCAA kukaa chini na kuona jinsi ya kuboresha mazingira ya mapango ya Amboni yawe ya kipekee na kuvutia zaidi.
“Nazungumza kwa niaba ya waheshimiwa wabunge ambao leo wametembelea eneo hili na kujionea kazi kubwa mnayoifanya katika kukuza utalii, ni jukumu lenu sasa kuhakikisha licha ya uwepo wa mapango haya lakini pia mnafanya kila jitihada kuwa na mazao mapya ya utaalii kwa kuwa eneo hili ni kubwa na linaruhusu shughuli nyingi za utalii”, alisema mheshimiwa Mnzava.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana aliwaeleza wabunge hao kuwa wizara yake itaendelea kusimamia maelekezo yote yanayotolewa na kamati ili kuhakikisha kuwa kila chanzo cha utalii kinachoanzishwa kinakuwa na tija kwa taifa.
Balozi Chana ameeleza kuwa wizara yake iliamua kukabidhi mapango hayo kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kuboresha uhifadhi, na kuyatangaza zaidi ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya Nchi.
Kwa upande wake Kamishna wa uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Elirehema Doriye aliwaambia wabunge wa kamati hiyo kuwa mamlaka imejipanga kuboresha eneo hilo kwa kuanzisha mazao mapya ya utalii ikiwemo makumbusho ya viumbe wa baharini, maeneo ya kupumzikia, mchezo wa kutembea na kamba “zip line” pamoja na huduma za nyingine za kijamii na kitalii katika eneo la mapango.
Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii mheshimiwa Dunstan Kitandula (Mb) Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo anayesimamia Uhifadhi CP Benedict Wakulyamba, menejimenti ya mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na watendaji wa wizara ya Maliasili na Utalii.
0 Comments