Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam Januari 29, 2025 liliwapata na kuwahoji wasichana wawili ambapo mmoja wa Miaka 16 Mwanafunzi wa Kidato cha Pili na mwingine Miaka 12 Mwanafunzi wa Darasa la saba wakazi wa Vijibweni Kigamboni Dar es Salaam kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo baada ya kutengeneza mazingira kuwa wametekwa na kwamba watekaji wanataka pesa.
Hayo yamebainishwa leo Februari 4, 2025 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
SACP Muliro amesema ufutiliaji ulifanywa na kufanikiwa kubaini watoto hao walipokuwa na baada ya mahojiano ya kina walikiri kutengeneza tukio hilo la uongo ili waweze kujipatia pesa kwa udanganyifu toka kwa wazazi wao baada ya kutoweka tarehe 26/01/2025 na kuelekea Longoni Beach ambapo walikesha hapo hadi tarehe 27/01/205 asubuhi na baadae kuelekea maeneo ya Tungi hadi walipokamatwa wakiwa wakizunguka. Jeshi linalaani vitendo hivyo vya watu vyenye lengo la kujipatia pesa kwa njia za udanganyifu.
Aidha, amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam katika kipindi cha mwezi Desemba hadi Januari 2025 katika kusimamia mifumo ya haki jinai Mahakamani baadhi ya watuhumiwa mbalimbali walipatikana na hatia ikiwa ni pamoja na Idrisa Rashid (35) Mkazi wa Kwembe Kimara alihukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la kubaka kwenye Mahakama ya Wilaya Kinondoni. Paul Elisha (37) mkazi wa Mbezi Beach kwenye Mahakama hiyo hiyo ya Kinondoni alihukumiwa kifungo cha Maisha jela kwa kosa la kubaka na Jackson Mgeta (34) mkazi wa Kawe alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana ili kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi ikiwa ni pamoja na kutekeleza falsafa ya ulinzi shirikishii ili kuzuia vitendo vya kihalifu.

0 Comments