PINDA: VETA IMETOA MCHANGO MKUBWA KATIKA TAIFA, asema imepiga hatua kwa kutoa wahitimu bora wanaouzika soko la ndani na nje



Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) jijini Dar es Saalaam.


Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda akiwa ametembelea moja ya banda na kujionea bunifu katika maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) jijini Dar es Saalaam.

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Mstaafu Kayanza Mizengo Pinda amesema Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) imetoa mchango mkubwa katika Taifa ambao haupaswi kubezwa bali kuimarishwa zaidi.

Amebainisha hayo leo Machi 20, 2025 akizungumza wakati wa mjadala wa wadau wa VETA kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka hyo yanayofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Pinda ameeleza kuwa VETA imepiga hatua kubwa kwakutoa wahitimu bora na wanaouzika katika soko la ajira nchini na nje ya nchi.

"Niukweli usiopingika kwamba Veta imetoa mchango mkubwa sana katika Taifa hili na mchango wake haupaswi kubezwa bali unapaswa kuimarishwa zaidi kwakuwa hakuna namna yoyote utakwepa ufundi stadi katika maisha yako kama binadamu,” amesema Pinda.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu ametumia fursa hiyo kuipongeza VETA  kwa kazi nzuri inayofanya kwani juhudi zake zimesaidia kuongezeka kwa viwango bora vya bunifu zinazobuniwa nchini zenye tija katika jamii kwani zamani bunifu nzuri zilikuwa zikifanywa na mataifa yaliyoendelea pekee.

“Hakika tulikotoka miaka 30 iliyopita hatukuweza kutengeza kazi nzuri na za kibunifu tulikuwa tukiziona katika mataifa yaliyoendelea lakini hatimaye sasa kila kitu kizuri na chakiufanisi hupatikana hapa nchini hongereni VETA," ameongeza Pinda.

Awali Pinda alitembelea mabanda mbalimbali ya VETA na kujionea kazi mbalimbali za kibunifu na kivumbizi ambapo ameipongeza Mamlaka hiyo kwa kuendelea kunoa vijana mahili katika nyanja mbalimbali za ufundi stadi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore amesema matunda ya VETA yanayoonekana leo hii yamechangiwa kwa namna moja ama nyingine na Waziri Mkuu Mstaafu Pinda wakati wa uongozi wake na kwamba yanapozungumzwa mafanikio ya Mamlaka hiyo  ni lazima atajwe yeye.

“Mzee wetu huyu alisimamia ipasavyo matunda ya VETA na leo hii amejionea mwenyewe namna ambavyo Veta ilivyo imarika, alikuwa akitushauri mambo kadha wa kadha ili kuhakikisha chuo kinafanikiwa katika utoaji wa huduma zake kwa jamii na taifa” amesema Kasore

Maadhimisho hayo yanafikia kilele kesho na yatahitimishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassani ambapo yalizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Machi 18, 2025.

Post a Comment

0 Comments