TUNATAKA MAJI SAFI NA SALAMA NCHINI, MIAKA 63 YA UHURU BILA MAJI INATOSHA



Chama cha ACT Wazalendo tunaungana na mamilioni ya Watanzania nchini kuitaka serikali kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama nchini. Leo Machi 22, 2025, tunapoadhimisha Siku ya Maji Duniani, ACT Wazalendo tunasimama kidete kupaza sauti kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania wanaoendelea kutaabika bila maji safi na salam, gharama kubwa ya maji, kukatika mara kwa mara na mgao wa maji usio kwisha.

Ni fedheha na aibu kwa taifa letu kwamba baada ya miaka 63 ya uhuru, wananchi bado wanalazimika kutembea kilomita nyingi kutafuta maji, huku Serikali ya CCM ikiendelea kutoa ahadi zisizotekelezeka! 
Takwimu zinashtua! Vijiji zaidi ya 3,000 havina maji ya bomba, maeneo yenye shida kubwa ya maji ni Kanda ya Ziwa ikijumuisha Mkoa wa Mara, Simiyu, Geita, maeneo mengine ni sehemu kubwa ya mkoa wa Singida, Dodoma, Manyara na Morogoro.  Huku mijini kama Dar es salaam, Tanga, Njombe, Mwanza na Pwani kumekuwa na mgao mkali wa maji.

Serikali inazidi kupunguza bajeti ya maji, kutoka asilimia 2.2 mwaka 2021 hadi 1.7 mwaka 2023/24 – jambo linalothibitisha kukosekana kwa dhamira ya kweli ya Serikali. Miradi mingi ya maji imekwama, huku mabilioni ya fedha za walipa kodi yakiliwa na mafisadi wanaolindwa na mfumo wa kifisadi wa CCM.

ACT Wazalendo tunasema inatosha! Serikali ichukue hatua kwa kuwawajibisha mara moja wahusika wote wa uzembe na ufisadi katika utekelezaji wa miradi ya maji.

Pia, Serikali kuanzia mwaka wa fedha 2025/26 iongezwe bajeti ya maji kufikia angalau 5% ya bajeti ya Serikali Kuu kwa miaka mitano mfululizo ili kumaliza kabisa tatizo hili. 

Vile vile, Kusimamia huduma za maji zinazotolewa na watu binafsi ili kudhibiti usalama wa maji na ghaama za huduma hiyo.

Imetolewa na;

Yasinta Cornely Awiti
Waziri Kivuli wa Maji- ACT Wazalendo
22 Machi 2025.

Post a Comment

0 Comments