NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kusitisha mara moja Ziara, Mikutano, Semina na Makongamano, yanayohusisha Wajumbe wa Vikao vinavyopigia kura za maoni wagombea kwa ngazi zote mpaka baada ya kura za maoni na kuwataka wanachama kuepuka vitendo vyovyote ambavyo ni kinyume cha katiba, kanuni na miongozo.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi, Dkt. Emmanuel John Nchimbi leo Juni 23, 2025 imeeleza kuwa CCM inaendelea na maandalizi ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wanachama watakaojitokeza kuomba kugombea nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kupitia CCM.
Aidha taarifa hiyo imesema mchakato wa ndani ya CCM utahusisha zoezi la Uchukuaji na urejeshaji wa fomu, Vikao vya awamu ya kwanza vya Uchujaji na uteuzi kwa ajili ya upigaji wa kura za maoni na kisha Vikao vya Uchujaji na Uteuzi wa mwisho wa Wagombea wa CCM kwa nafasi husika.
“CCM inawataka Viongozi, Watendaji na Wanachama wake kuendelea kusimamia Maadili na Nidhamu ya Chama wakati wote wa Maandalizi ya mchakato wa ndani na utekelezaji wa shughuli za uteuzi wa wagombea wa CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.”
“Ni wajibu wa kila Mwanachama wa CCM kuendelea kuimarisha Umoja na Mshikamano ndani ya Chama kwa kuzingatia dhamana na imani kubwa tuliyopewa na Watanzania.”—imesema taarifa hiyo ya CCM.

0 Comments