NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo Mpogolo amelipongeza Baraza la Madiwani kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
DC Mpogolo ametoa pongezi hizo leo Juni 20, 2025 wakati wa uvunjaji rasmi wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambapo ameeleza kuwa wao ndio sababu ya mafanikio yaliyopo sasa na kwamba miradi hiyo inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Ametumia fursa hiyo kuwatoa wasiwasi wananchi wa Jiji hilo kwa kuwahakikishia kuwa miradi ya maendeleo inayokaribia kukamilika itatekelezwa na kukamilishwa kwa wakati kama ilivyopangwa.
Ameeleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam chini ya Mkurugenzi Mabelya ina watendaji makini, wenye maono na wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi na uwajibikaji mkubwa katika kusimamia maendeleo ya wananchi.
"Tuna imani kubwa na uongozi wa Mkurugenzi Mabelya pamoja na timu yake ya wataalamu. Wanajituma, wanafanya kazi kwa uaminifu na wamejipanga kuhakikisha miradi yote inaisha kwa ubora unaostahili," amesema DC Mpogolo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji hilo Elihuruma Mabelya, ametoa salamu za pongezi na shukrani kwa Madiwani wote kwa kazi kubwa na mchango wao katika kuleta maendeleo ya Jiji hilo katika kipindi chao cha uongozi.
Amesema kuwa kipindi cha uongozi wa Baraza hilo kimeacha msingi imara wa maendeleo, na kwamba Halmashauri itaendelea kusimamia kwa dhati utekelezaji wa maazimio yote yaliyopitishwa na Baraza hilo.
Amesisitiza kuwa Halmashauri itaendelea kusimamia miradi yote ya maendeleo kwa uwazi na kwa kushirikisha jamii, huku akiwasihi Madiwani waliomaliza muda wao kuendelea kuwa sehemu ya harakati za maendeleo katika kata zao kama wazalendo na mabalozi wa mabadiliko.
“Tutaendeleza kazi na misingi mema mliyoiacha kwa maslahi ya wananchi. Baraza limevunjwa, lakini dhamira ya kuwatumikia wananchi haijawahi kuvunjwa. Tunawaaga kwa heshima, tukijivunia kazi yenu, na tukiahidi kuendeleza misingi hiyo kwa uaminifu,” amesema Mkurugenzi Mabelya.
Naye, Mstahiki Meya, Omary Kumbilamoto, amewashukuru Mkuu wa Wilaya ya Ilala pamoja na watendaji wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chote cha uongozi wake. Amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya mshikamano, maono ya pamoja, na juhudi za pamoja kati ya Baraza la Madiwani na watendaji wa Halmashauri.
Hatua ya kuvunjwa kwa Baraza hilo la Madiwani inatekeleza agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, aliyeagiza Halmashauri zote nchini kuvunja mabaraza ya madiwani ifikapo Juni 20, 2025, kufuatia kumalizika kwa muda wa kisheria wa uongozi wa Serikali za Mitaa.
Kwa sasa, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itasimamiwa na Mkurugenzi wa Jiji, Elihuruma Mabelya, pamoja na wataalam wa Halmashauri hadi pale Baraza jipya la Madiwani litakapoundwa baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 2025.





0 Comments