#KAZIINAONGEA
Kuna miradi inayojengwa kwa saruji na nondo, lakini kuna mingine inayoandikwa kwa imani, matumaini na historia ya Taifa. Mnamo Juni 19, 2025, Tanzania iliandika ukurasa mpya wa maendeleo kwa uzinduzi rasmi wa Daraja la J.P. Magufuli, lililojengwa kati ya Kigongo na Busisi, mkoani Mwanza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa amesimama juu ya daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3 na barabara unganishi ya kilomita 1.66, alizungumza si kwa takwimu tu bali kwa sauti ya kiapo alichoweka miaka minne iliyopita, kuendeleza kila wazo, kila jiwe na kila jasho lililomwagwa na watangulizi wake.
“Miongoni mwa vitu nilivyoahidi ni kuendeleza miradi iliyoanzishwa na watangulizi wangu,” amesema kwa sauti ya uwajibikaji, huku upepo wa Ziwa Victoria ukivuma pembeni yake.
Daraja hili si tu kiungo cha Wilaya za Misungwi na Sengerema bali ni alama ya kutimia kwa ahadi, kwa sababu ujenzi wake ulipoanza mwaka 2019, ulikuwa umekwama kwenye asilimia 25 pekee. Katika kipindi cha miaka minne tu, chini ya uongozi wa Rais Samia, limekamilika kwa ubora wa Kimataifa na kwa kutumia fedha za ndani pekee, zaidi ya shilingi bilioni 718 zikitumika bila kuchukua mkopo kutoka nje ya nchi.
Kwa sasa, wananchi wanatumia dakika nne pekee kuvuka sehemu ambayo zamani walihangaika kwa saa kadhaa kutumia vivuko vya majini. Hilo pekee ni mapinduzi ya kiuchumi kwa Kanda ya Ziwa.
“Tanzania sasa ina uwezo wa kupanga na kutekeleza miradi mikubwa. Asilimia 92 ya waliotekeleza ujenzi huu ni Watanzania,” amesema Rais Samia kwa fahari.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisimama mbele ya hadhira na kupongeza juhudi za Rais akisema,
“Hongera Mheshimiwa Rais kwa bidii yako ya kutafuta fedha kukamilisha miradi ya miundombinu. Hakika umefanya kazi kubwa.”
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameikumbusha hadhira kuwa ujenzi huu ulikwama kwa miaka mingi, lakini uongozi wa Dkt. Samia uliutoa shimoni,
“Dkt. Samia alilikuta daraja likiwa asilimia 25, fedha zilizolipwa zilikuwa Bilioni 152 tu. Leo, kila senti imeshalipwa, kila jiwe limewekwa, na kazi imekamilika.”
Lakini uzito wa daraja hili hauishii kwenye namba na vifaa vya ujenzi. Kwa mujibu wa taarifa ya Rais kupitia mtandao wake wa kijamii, ameeleza:
“Leo ni siku ya kihistoria kwa nchi yetu na Ukanda wa Afrika Mashariki.Tumefungua ukurasa mpya katika sekta ya usafiri kwa kuzindua Daraja la JP Magufuli. Daraja hili ni uthibitisho kuwa tunaweza kupanga na kutekeleza mambo makubwa.”
Daraja la J.P. Magufuli sasa linajulikana kuwa la saba kwa urefu barani Afrika, likitanguliwa na madaraja mawili kutoka Misri, moja Nigeria, mawili kutoka Msumbiji na moja kutoka Morocco. Zaidi ya kuwa kivuko cha ndani, daraja hili linaiunganisha Tanzania kiuchumi na mataifa jirani kama DRC, Rwanda, Burundi na Uganda kupitia barabara ya Usagara - Sengerema - Geita.
Kwa kuona umuhimu wake kimkakati, Rais Samia ameiagiza Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na TANROADS na vyombo vya ulinzi kuhakikisha linafanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara na kulindwa kwa niaba ya Watanzania wote.
Mbali na hilo, Serikali pia imepanga kujenga barabara ya njia nne kati ya Mwanza mjini na Usagara (km 22), huku vivuko vya zamani vitatu vikihamishiwa maeneo mengine ya Ziwa Victoria ili kuendeleza huduma kwa wananchi wengine.
Katika ulimwengu wa habari, simulizi ya daraja hili limevuka mipaka ya Tanzania. Mwandishi Pauline Odhiambo kutoka TRT Afrika ameliita “daraja la kipekee linaloonesha uthubutu wa Taifa” – akisisitiza kuwa Afrika nzima, na hata Ulaya, sasa inaelewa Tanzania imejenga si daraja tu, bali imani.
Hakika Daraja hili limejengwa juu ya maji, lakini limeinua mioyo ya watu. Kama Taifa, tumeshuhudia si ujenzi wa miundombinu tu, bali pia ujenzi wa matumaini. Rais Samia ameonesha kuwa si lazima upige kelele ili kazi ijulikane, bali kazi ikikamilika itaongea, na sasa Taifa linasimama na kushuhudia.
Hivyo ni zamu ya wananchi kulipa imani hiyo kwa vitendo. Oktoba si tarehe tu, bali ni jukwaa la heshima.
Ni siku ya kuonyesha mioyo ya shukrani, ni siku ya kukubali kwa vitendo juu ya yote yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan.
*#KazinaUtuTunasongaMbele*

0 Comments