Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila (Kulia) akikabishiwa jiko linalotumia umeme kidogo na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Lazaro Twange (kushoto) jijini Dar es Salaam.
Habari mbalimbali katika picha kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ajili ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na Ubungo jijini Dar es Salaam.
NA ABRAHAM NTAMBARA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Altbert Chalamila amewataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kutoka Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ubungo kuwa mabalozi wa kueleza huduma nzuri zinazotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
RC Chalamila ametoa kauli hiyo leo Juni 24, 2025 wakati akifungua kikao kazi kilichoandaliwa na TANESCO kwa ajili ya Wenyeviti wa Serikali za mitaa kutoka Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ubungo kilichofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.
Amebainisha kuwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ni wadau muhimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali kwa kuwa miradi hutekelezwa katika maeneo yao ya kiutawala.
Kwamba hata miradi mingi ya TANESCO iko kwenye mitaa yao hivyo amesema "Ni imani yangu kuwa kupitia kikao kazi hiki wenyeviti wote wanakwenda kuwa mabalozi wa kueleza huduma nzuri zinazotolewa na TANESCO pia kulinda miundombinu ya Shirika hili,".
Mkuu hiyo wa Mkoa ametumia fursa hiyo kuipongeza TANESCO kwa kuona umuhimu wa kukutana na kundi hilo muhimu ili liweze kufahamu kwa kina majukumu ya shirika hilo lakini pia kutoa mawazo na ushauri wa namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma za nishati ya umeme kwa wananchi hususani katika mitaa yao.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange amesema Shirika hilo kwa kutambua kuwa Wenyeviti wa Serikali za mitaa ni wadau muhimu wakaona waandae kikao kazi kwa ajili yao ili kutengeneza mfumo mzuri wa mawasiliano ambao utatusaidia kujua wananchi wanasemaje kuhusu huduma za TANESCO pia wenyeviti wawe na uwezo wa kuelewa nini kinafanywa na shirika pamoja na kuwaelimisha wananchi walioko katika maeneo yao.
Twange ametumia fursa hiyo kumkabidhi RC Chalamila na Viongozi wachache wa Mitaa majiko ya Umeme ambayo yanatumia umeme kidogo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
0 Comments