NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemevu wa Hamashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha ili kuendesha biashara kwa tija na kuhakikisha urejeshaji wa mikopo unafanyika kwa wakati ili kuwafikia wananchi wengine.
Kauli hiyo DC Mpogolo ameitoa leo Juni 20, 2025 akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo isiyo na riba iliyofanyika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam ambapo amepongeza juhudi za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kuimarisha utoaji wa mikopo hiyo.
Mheshimiwa Mpogolo ameeleza kuwa mikopo hiyo ni chombo muhimu cha kufanikisha maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.
DC Mpogolo ameeleza kuwa mapato yaliyokusanywa na Halmashauri yameongezeka, hali iliyoleta mabadiliko makubwa katika uwezo wa Jiji kutoa mikopo kwa walengwa.
“Fedha hizi si msaada ni haki ya wananchi waliopo kwenye mpango huu wa kisheria. Rais wetu ameweka mazingira wezeshi, sisi kama viongozi ni lazima tusimame imara kuhakikisha fedha hizi zinawafikia walengwa kwa uaminifu na bila urasimu,” amesema DC Mpogolo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji hilo Elihuruma Mabelya amesema Halmashauri hiyo imetenga zaidi ya shilingi bilioni 18 kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo kwa vikundi 945 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu katika mwaka huu wa fedha 2024/2025.
Mabelya amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa sauti na nguzo kubwa ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyokuwa na riba inayotolewa na Halmashauri kwa mujibu wa sheria.
“Kazi kubwa tuliyonayo sasa ni kurahisisha utoaji wa mikopo hii na kuhakikisha hakuna changamoto kwa waombaji. Tumejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kuunda vikundi, kuomba mikopo, na kuhakikisha wanarejesha kwa ufanisi. Hatua hizi ni sehemu ya kuhakikisha tunatimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri,” amesisitiza Mabelya
Aidha, Mkurugenzi Mabelya amewatoa hofu wananchi kuhusu upatikanaji wa mikopo hiyo, akisisitiza kuwa fedha zipo na zitawafikia wanufaika wote waliokidhi vigezo, ili mikopo hiyo iweze kuchangia katika kuongeza kipato cha familia na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mikopo hiyo itatolewa kupitia mfumo wa kibenki, ambapo Benki ya CRDB na Benki ya NMB zimepewa jukumu la kusimamia utoaji wa fedha kwa vikundi vilivyoidhinishwa. Mfumo huu unalenga kuhakikisha uwazi, usalama wa fedha, na ufuatiliaji mzuri wa urejeshaji wa mikopo.
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kutenga zaidi ya shilingi bilioni 22 kwa ajili ya mikopo hiyo, ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuinua kundi kubwa la wananchi kupitia uchumi jumuishi.



0 Comments