KATIBU MKUU WA WMO AAHIDI KUSHIRIKIANA NA TMA KUBORESHA HUDUMA ZA HALI YA HEWA



Na Mwandishi Wetu, Geneva

KATIBU Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Profesa Celeste Saulo ameahidi kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuboresha huduma za hali ya hewa kwa matumizi katika sekta za kiuchumi na kijamii.

Ameyasema hayo wakati wa kikao baina yake na Dk. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambaye pia ni Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika WMO na Makamu wa Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) wakati wa kikao cha 69 cha Kamati Kuu Tendaji ya IPCC (Intergovernmental Panel on Climate Change jijini Geneva, Uswisi.

Kikao hicho kilikuwa na lengo la kujadiliana kuhusu maendeleo ya utoaji wa huduma za hali ya hewa na mipango ya kuendeleza ushirikiano.

Profesa Saulo ameipongeza TMA kwa uwekezaji mkubwa hususan katika miundombinu ya kisasa ya hali ya hewa na kwa kuendelea kufanya vizuri katika utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini pamoja na kusaidia nchi nyingine katika sekta ya hali ya hewa.

Profesa Celeste Saulo ameahidi kuendelea kusaidia katika kuboresha huduma za hali ya hewa na mafunzo kwa wataalamu wa hali ya hewa kupitia programu mbalimbali za WMO ikiwemo eneo la mafunzo ya akili mnemba.

Aidha, Profesa Saulo amesisitiza kuwa, Taasisi za Hali ya hewa za nchi wanachama ndizo zenye jukumu mahsusi la kutoa huduma za hali ya hewa katika nchi wanachama wa WMO hivyo uwekezaji katika sekta hii utaboresha zaidi huduma kwa jamii.

“ Taasisi za hali ya hewa kama TMA ndizo zenye jukumu mahsusi na chanzo cha kuaminika cha huduma za hali ya hewa kwa mujibu wa miongozo ya WMO na napongeza TMA kwa kuendelea kutumia vyema uwekezaji na kutoa huduma bora za hali ya hewa.

Pia napongeza TMA kwa kuwa mstari wa mbele kusimamia vyema programu za WMO na kusaidia nchi nyingine kikanda ili kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa katika nchi zao na kikanda,” alisema Profesa Saulo.

Katika Kikao hicho, Dk. Chang’a ameeleza dhamira ya TMA ya kuboresha huduma za hali ya hewa na kusimamia vyema programu za WMO zinazotekelezwa nchini na kikanda.

“TMA itaendelea kutoa wataalamu wake mahiri kuchangia katika utekelezaji wa programu mbalimbali za WMO kwa manufaa ya dunia nzima na tutaendelea kusaidia wenzetu hasa katika kanda ya Afrika kwa uzoefu na utaalamu tulio nao, kwa msaada wa WMO na uwekezaji mkubwa wa serikali katika tasnia ya hali ya hewa nchini,” alisema Dk. Chang’a.

Aliimjulisha Katibu Mkuu wa WMO kuwa, Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi wanachama wa WMO ambazo wataalamu wa TMA wametoa msaada wa kiufundi barani Afrika hivi karibuni ni Lesotho, Namibia, Burundi, Zimbabwe na Sudan Kusini, ambapo nchi hizo waliwezeshwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya uboreshaji wa mfumo wa usimamizi wa ubora wa huduma, utabiri wa hali mbaya ya hewa, utabiri wa hali ya hewa kwa kutumia modeli za kihesabu na kompyuta.

“Tuiwapitisha pia kwenye mchakato wa kisheria katika sekta ya hali ya hewa na usambazaji wa huduma za hali ya hewa kwa umma,” alisema Dk. Chang’a.

Post a Comment

0 Comments