WAZIRI MKUU: VIONGOZI WA MIKOA NA WILAYA SIMAMIENI KILIMO NA UFUGAJI ENDELEVU KULINDA MTO THE GREAT RUAHA


Na. Happiness Sam- Ruaha

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa mikoa na wilaya zinazozunguka bonde la Usangu kusimamia na kuratibu vizuri shughuli za kilimo na ufugaji endelevu ili kudhibiti uharibifu wa mazingira ambao ni kichocheo kikuu cha kupungua kwa mtiririko wa maji katika Mto The Great Ruaha na kuathiri ikolojia ya hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini Tanzania.

Ameyasema hayo leo Julai 5, 2025 wakati wa uzinduzi na ushiriki wa mbio za The Great Ruaha Marathon zilizofanyika eneo la Ibuguziwa lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha zikihusisha mbio za Kilometa 21, 10 na 05.

Akiwa katika eneo hilo la Ibuguziwa kando ya mto The Great Ruaha Waziri Majaliwa alisema, “Ni wajibu wa viongozi wa mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa wafugaji na wakulima kutoendelea kufuga na kulima kiholela kunakochangia kuharibu maeneo mengi yenye vyanzo vya maji yanayotiririkia katika bonde la Usangu na kujikusanya katika ardhi oevu ya Ihefu kilipo chanzo cha Mto  The Great Ruaha.”

Aidha, Waziri Majaliwa aliongeza, “Mbio za The Great Ruaha Marathon mbali na kukuza utalii wa ndani na nje pia zimelenga kujenga uelewa kwa wananchi kulinda na kuhifadhi maliasili zetu wakiwemo wanyamapori, ndege, wadudu na mimea ya aina mbalimbali. Kwa kulinda tunu hizi tutakuwa tumewaachia watoto na wajukuu wetu wajao urithi mkubwa sana.”

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James akimkaribisha Waziri Mkuu alisema, “Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na viwanja vya ndege vilivyomo ndani ya hifadhi na kile cha Nduli kilichopo mjini Iringa ili kuhakikisha wageni wanaoingia ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha wanafika kwa urahisi, hivyo kama wadau wa utalii tuendelee na jitihada za kukaribisha wageni kwa wingi kwani mazingira yapo safi na utalii upo vizuri.”

“Mbio hizi zimeandaliwa kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko Kusini mwa Tanzania, Hifadhi ya Taifa Ruaha ikipewa kipaumbele kulingana na baioanuai zilizomo. Hifadhi hii imejaliwa kuwa na wanyamapori na mandhari nzuri ambazo zimeendelea kuvuta watalii wengi, na hili limedhihirika baada ya kila mwaka idadi ya watalii kuendelea kuongezeka,” aliongeza James.

Awali, akiukaribisha ugeni huo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA (T) Musa Nassoro Kuji alisema, “ Leo tunashiriki mbio hizi kwa mara ya nne mfulululizo huku hamasa na idadi ya washiriki ikiongezeka kila mwaka, hivyo TANAPA itaendelea kuhakikisha mbio hizi zinaendelea kuwepo kila mwaka pia zinafikia viwango vya kimataifa.”

“ Tutaendelea pia kulinda na kuhifadhi mto The Great Ruaha kwani ndio kitovu cha Uhifadhi na Ikolojia ya hifadhi hii, tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaokaa pembezo wasiharibu vyanzo hivyo ili mto huu uendelee kutiririsha maji kwa mustakabali wa hifadhi hii na Taifa kwa ujumla”, aliongeza Kamishna Kuji.

Mbio hizo za “The Great Ruaha Marathon” zilizofanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha zimeshirikisha wanamichezo kutoka maeneo mbalimbali nchini huku washiriki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wakiibuka kidedea kwa mbio za kilometa 10 ambapo mshindi wa kwanza akiwa ni Askari Uhifadhi Daraja la Tatu - Elibariki Buko kutoka TANAPA na mshindi wa pili ni Michael Kalay kutoka TFS.

Post a Comment

0 Comments