WIZARA YA NISHATI YAANZA KUFANYIA KAZI MAAGIZO YA RAIS SAMIA KUHUSU NISHATI YA NYUKLIA



*Dkt.Kazungu asema Wizara ya Nishati itasimamia ipasavyo utekelezaji wa maagizo ya Rais

 *Asisitiza lengo ni kuwa na nishati salama na ya kudumu

#KAZIINAONGEA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu ameongoza kikao kazi maalum kilicholenga kujadili hatua za utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu maandalizi ya kuanzisha matumizi ya nishati ya nyuklia nchini katika kuzalisha umeme.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam kimehudhuriwa na Watendaji waandamizi kutoka Wizara ya Nishati, Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara,  Wawakilishi kutoka mashirika ya udhibiti pamoja na wataalam wa Sekta ya Nishati na Mazingira nchini.

Dkt. Khatibu Kazungu ameeleza kuwa, Wizara ya Nishati itasimamia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia aliyoyatoa wakati akihitimisha shughuli za Bunge tarehe 27 Juni 2025 kuhusu matumizi salama ya nishati ya nyuklia nchini katika kuzalisha umeme..

“Wizara ya Nishati itaendelea kusimamia mchakato wa uanzishaji wa mpango wa nishati ya nyuklia ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa na uhakika wa nishati salama na ya kudumu. Tutaendelea kushirikiana na taasisi zetu na wadau wengine kuhakikisha maandalizi haya yanafanyika kwa umakini mkubwa, kwa kufuata viwango vya kimataifa.” Amesema Dkt. Kazungu

Aidha, Dkt. Kazungu ameiagiza Kamati ya Kitaifa inayoshughulikia suala hilo,  kuandaa ramani ya kitaifa (National Roadmap) itakayoonesha hatua zote muhimu za utekelezaji wa mpango wa nyuklia, kuanzia sasa hadi kufikia mwaka 2050.

Amesema kuwa, mpango wa matumizi ya  nyuklia unahusisha upembuzi yakinifu wa malighafi za uranium zilizoko nchini, tathmini za kisera na kisheria, uhamasishaji wa umma pamoja na maandalizi ya kisera kwa ajili ya uwekezaji wa nishati hiyo.

Naye Kamishna wa Umeme na Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Innocent  Luoga amesisitiza kuhusu umuhimu wa kujenga misingi ya uelewa wa kitaifa kuhusu nishati ya nyuklia.

“Tunapaswa kuwekeza katika maarifa na uhamasishaji, ili wananchi waelewe kuwa nyuklia si tishio, bali ni fursa,  tunahitaji kutoa elimu kuhusu manufaa ya nishati ya nyuklia, namna ya udhibiti wake, na hatua za tahadhari zinazochukuliwa kimataifa kuhakikisha kunakuwa na mazingira salama wakati wote."  Amesema Kamishna Luoga

*#KazinaUtuTunasongaMbele*

Post a Comment

0 Comments