*Watumishi Wahamasishwa kupiga kura Oktoba 29 kwa Maendeleo ya Sekta ya Madini*
Dodoma*
Wizara ya Madini leo Oktoba 18, 2025, imeshiriki Bonanza la Michezo lililofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlin jijini Dodoma, likiwakutanisha watumishi kutoka taasisi zote za Wizara. Bonanza hilo limekuwa sehemu ya utaratibu wa kila robo mwaka ulioanzishwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, kwa lengo la kujenga mshikamano, afya bora, na kuimarisha ari ya watumishi kuweza kuitumikia Serikali ipasavyo.
Akizungumza katika bonanza hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba amesema michezo ni nguzo muhimu ya kuimarisha umoja, afya za watumishi ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza ili waweze kuishi maisha marefu na hatimaye kuongeza ufanisi kazini na kutimiza malengo iliyowekewa Wizara na Serikali.
Aidha, amewahimiza watumishi wote kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura ili, kuchagua viongozi bora wenye dira ya kuweza kuisimamia Sekta ya Madini kwa maendeleo ya sekta na maendeleo kwa taifa kwa ujumla kwa kusikiliza sera na kuwahamasisha wengine na hatimaye kuwachagua viongozi wanaofaa.
Pia, amezitaka taasisi zote chini ya wizara hiyo kuendelea kufanya kazi kwa tija na matokeo, ili kuiheshimisha Sekta mbele ya watanzania na jumuiya ya kimataifa, kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa ushauri, tafiti na mitambo na kuendelea kuhamasiaha uwekezaji nchini kwa kutoa taarifa za uwazi na uwajibikaji kwa kampuni za madini.
‘’Niendelee kuwapongeza sana taasisi zote, Tume ya madini kuendelea kutuheshimisha kwenye makusanyo, STAMICO kuendelea kuwaelea wachimbaji wadogo, kuwapata ushauri na mitambo na kuwa nao karibu, GST kuendelea kuwasaidia wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo kwenye masuala ya kijiolojia, TEITI kuendelea kutoa taarifa kwa uwazi kwenye sekta ya Madini ili wananchi wafahamu mwelekeo na imechangia kitu gani na kikubwa zaidi kuwavutia wawekezaji kuhusu wazi na usimamizi wa rasilimali madini,’’ amesema Eng. Samamba.
0 Comments