Jumla ya
wanafunzi 5,188 wa Darasa la Nne wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Upimaji wa
Kitaifa katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido, mkoani Arusha kuanzia kesho
Oktoba 22 hadi 23, 2025.
Akizungumza
leo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mkuu wa Idara ya
Utawala na Utumishi, Bw. Peter Matemba, amesema maandalizi yote muhimu
yamekamilika huku wanafunzi wakiwa tayari kwa mtihani huo muhimu katika safari
yao ya kielimu.
“Kama wilaya
tumejipanga vizuri, wanafunzi wameandaliwa vya kutosha. Tunawaomba wazazi
wawaandae watoto wao vizuri na kuhakikisha wanafika shuleni mapema kwa ajili ya
kufanya mtihani. Vilevile, tunatoa wito kwa wanafunzi wenyewe kujiandaa kwa
bidii,” alisema Bw. Matemba.
Kati ya
watahiniwa hao, wavulana ni 2,726 na wasichana 2,462. Mtihani huo utafanyika
katika shule 70, zikiwemo shule 57 za serikali na 13 zinazomilikiwa na
mashirika ya dini pamoja na shule binafsi.
Bw. Matemba
aliongeza kuwa walimu wakuu wameelekezwa kuandaa mazingira rafiki kwa ajili ya
mtihani huo na kwamba semina mbalimbali zimefanyika kwa ajili ya kuwaandaa
wasimamizi wa mitihani kuhakikisha uendeshaji wake unafanyika kwa ufanisi.
"Maandalizi
yote muhimu tumeyakamilisha. Tunawatakia heri na baraka wanafunzi wetu wote
katika upimaji huu wa kitaifa," aliongeza.
“Naomba
wazazi wawaruhusu watoto wao kufika shuleni kwa wakati, na kwa wanafunzi nawahimiza
wajibu mitihani yao kwa kuzingatia yale waliyojifunza kutoka kwa walimu wao,”
alisema Mwalimu Bunonus.
Mtihani huu wa Upimaji wa Kitaifa ni kipimo muhimu cha kutathmini uwezo wa wanafunzi na kuandaa msingi bora kwa maendeleo yao ya kitaaluma.

0 Comments