ZITTO ATAKA KILA MWANANCHI APATE MATIBABU BILA KIKWAZO CHA KIPATO, KIGOMA




NA MWANDISHI WETU

Mgombea ubunge jimbo la Kigoma mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewaahidi wananchi kuwa endapo chama hicho kitashinda nafasi ya ubunge na udiwani katika kata za jimbo hilo, kitakuja na mkakati utakaohakikisha kila mwananchi anapata matibabu bora pasipo kujali kipato chake.  

Akizungumza jana, Oktoba 17, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye kata ya Kasimbu jimboni hapo mkoani Kigoma, Zitto amesema mfumo wa huduma za afya nchini uliojengwa na chama cha CCM hautoi matibabu inavyostahiki kwa wananchi.

Akiwa katika kampeni za nyumba kwa nyumba, Zitto alipata nafasi ya kuwatembelea wagonjwa mbalimbali katika kata hiyo, ambapo alikuta baadhi ya wagonjwa wakiwa wamelala majumbani kwao pasipo kuwa na matumaini ya kupata matibabu kutokana na hali duni ya kipato cha familia hizo.

“Nimepita kumuona binti mmoja mgonjwa jirani na shule ya msingi Karuta ni mgonjwa kweli kweli lakini kutokana na hali ya kipato ya familia amelala ndani tu, na hana matumaini yoyote yale ya matibabu”, alisema Zitto

Amesema mfumo wa huduma za afya uliopo umekuwa ukisababisha watu kupoteza maisha hata pale wanapoumwa magonjwa yanayoweza kutibika kutokana na mfumo huo kuwajali zaidi wananchi wenye kipato cha juu pekee.

Zitto amesema licha ya kutokuwa mbunge wa jimbo hilo katika kipidi cha miaka minne iliyopita ofisi yake iliweza kutoa msaada kwa wagonjwa 143 waliotibiwa bure kutoka katika Manispaa ya Kigoma Ujiji. 

“Watu wengi nilikuwa nawapa huduma siwajui, napigiwa simu kuna mgonjwa yupo Kipampa ana rufaa ya kwenda muhimbili, mwingine yupo Mwanga kusini ana rufaa ya kwenda Bugando nawaambia leteni ‘control number’ wengi siwajui”, alisema Zitto

Aliongeza kuwa endapo chama chake kikiongoza manispaa hiyo atarejesha mpango aliowahi kuutumia kati ya mwaka 2005 hadi 2010 akiwa mbunge, ambapo alitenga asilimia 50 ya fedha za mfuko wa mbunge kuchangia watu wanaolipia NSSF ili kupata huduma ya bima ya afya.

“Tunataka tujenge manispaa ambayo itakuwa ni mfano,manispaa ambayo raia wake akipata ugonjwa wa aina yoyote awe ana uhakika atapata matibabu, kama kufariki iwe ni kwa amri ya Mungu lakini siyo apoteze maisha kwa kuwa tumeshindwa kumtibu,” aliongeza Zitto

Naye mgombea udiwani wa kata ya Kasimbu wa chama hicho, Juma Mzee akizungumza katika mkutano huo wa kampeni aliahidi atahakikisha anashughulikia suala la upimaji ardhi katika kata hiyo ili kurasimisha ardhi kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments