BARAZA LA WAFANYAKAZI WIZARA YA NISHATI LAJENGEWA UELEWA KUHUSU DIRA 2050, nishati ni moja ya vichocheo vya Dira 2050





Waelimishwa pia kuhusu mafao ya PSSSF na usalama wa kifedha

NA MWANDISHI WETU

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati wamejengewa uelewa kuhusu mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya taifa kuelekea maendeleo ya muda mrefu na endelevu.

Akizungumza Desemba 16, 2025 mkoani Morogoro, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Bw. Titus Kaguo, amesema kuwa kufuatia kukamilika kwa Dira ya 2025, taifa linaelekea katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2035 na uchumi wa kipato cha juu ifikapo mwaka 2050.

"Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 (Tanzania Development Vision 2025) ilikuwa mpango wa maendeleo wa muda mrefu wa miaka 25 ulioliongoza taifa katika kufikia uchumi wa kipato cha kati na kuweka msingi wa maendeleo ya kisasa.Dira hiyo ilijikita katika sekta muhimu ikiwemo nishati, kilimo, viwanda, miundombinu na teknolojia, ambazo zimekuwa nguzo kuu za maendeleo ya taifa." Amesema Kaguo

Ametaja vichocheo vya Dira 2050 kuwa ni nishati, usafirishaji fungamanishi, sayansi na teknolojia, utafiti na maendeleo pamoja na mageuzi ya kidijitali

Aidha, wajumbe hao pia walipatiwa elimu kuhusu mafao yanayotolewa na Mfuko wa Pensheni, Akiba na Hifadhi ya Jamii (PSSSF), ambayo ni nguzo muhimu ya ustawi wa watumishi wa umma.

Mafao hayo ni pamoja na pensheni ya uzeeni, mafao ya ulemavu, ajali, uzazi, ugonjwa, mafao ya wafiwa pamoja na msaada wa mazishi. Kupitia mafao hayo, watumishi wa umma na familia zao hupata usalama wa kifedha katika nyakati za dharura na kipindi cha baada ya kustaafu, hatua inayochangia kuboresha maisha na kuimarisha uhakika wa mustakabali wa kifedha.

Post a Comment

0 Comments