DED LONGIDO AKABIDHI GARI IDARA YA FEDHA KUONGEZA UKUSANYAJI MAPATO YA HALMASHAURI





NA ABRAHAM NTAMBARA, LONGIDO

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Nassoro Shemzigwa, leo Desemba 5, 2025, amekabidhi gari jipya aina ya Toyota Land Cruiser kwa Idara ya Fedha, Sehemu ya Mapato, kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bw. Shemzigwa amesema kuwa gari hilo limegharimu shilingi milioni 226.2, fedha za mapato ya ndani, na lengo ni kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ili kuongeza uwezo wa Halmashauri kutoa huduma bora kwa wananchi wa Longido.

“Gari hii imenunuliwa kwa shilingi milioni 226.26, fedha za mapato ya ndani, na tunaikabidhi Idara ya Fedha – Sehemu ya Mapato. Tunaamini gari hii itasaidia kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri. Muende mkafanye kazi, mkusanye mapato,” amesema Bw. Shemzigwa.

Kwa upande wake, Afisa Mapato wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Chathbert Njau, amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji na Menejimenti ya Halmashauri ya Longido kwa kuwapatia gari hilo.

Bw. Njau amebainisha kuwa kwa muda mrefu Idara ilikuwa haina gari la uhakika kwa ajili ya shughuli za ukusanyaji wa mapato. Amehakikishia uongozi kwamba gari hilo litatumika kwa ajili ya kazi za ukusanyaji wa mapato pekee.

Ameongeza kuwa kupatikana kwa gari hilo kutasaidia kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato ili kuboresha zaidi huduma kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments