MBETO: HEKO WATANZANIA KWA KUPUUZA WITO WA MADALALI WAUZA UMOJA NA AMANI



Na Mwandishi  Wetu,  Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi  kimesifu msimamo wa  watanzania  kwa   kuwapuuza mamluki na vibaraka wachache  wanaotumiwa na mabeberu kuvuruga ustawi wa  Amani, Umoja na Mshikamano  wa Kitaifa . 

Kimekitaja  kitendo cha Wananchi  kuonyesha Utii wa Sheria na kutojitokeza katika maandamano haramu Disemba  9 Mwaka huu,  kimefikisha ujumbe kuwa Watanzania kamwe hawatagawanyika. 

Katibu  wa Kamati  Maalum  ya NEC Zanzibar,  Idara  ya Itikadi  ,Uenezi na Mafunzo,  Khamis  Mbeto  Khamis  , ameeleza hayo na kuwataja Watanzania walikataa , wamekataa na wataendelea kukataa kuuza utu wao  au kupoteza heshima ya Taifa lao.

Mbeto  aliwashukuru  Watanzania  kwa uamuzi huo unaodumisha  Amani  na utulivu ,ukiwasuta vibaraka  wanaonunulika kwa kulipwa  ujira wa Fedha zenye  dhambi   ili  wachochee machafuko nchini.

Alisema njia pekee bora na sahihi    ni  serikali  kuendelea na mkakati wake wa kuzitafutia tiba changamoto zinazowakablii wananchi ,  kuboresha huduma za jamii na  kupata mbinu  mbadala zitakazotanua wigo wa  Ajira kwa Vijana. 

"Watanzania  kwa Umoja na Mshikamano  wao wamewatumia ujumbe vibaraka wachache waliodhani wangefanikiwa  kuwagawanya. Kwa nguvu  ya  Uzalendo,   Utaifa walionao,wamechagua   kulinda heshima na kukataa kugawanyika " Alisema Mbeto 

Aidha, Katibu  huyo Mwenezi  aliongeza kusema  kwa namna  yeyote ile, Watanzania wataendelea  kuthamini Taifa lao, umoja wa kitaifa  wa  nchi zao kwani  watanzania wamekuwa wakiishi kwa maelewano  kwa miaka zaidi  ya sitini.

"Ahadi  na kazi ya CCM ni kuzisukuma Serikali  ziteleleze wajibu wa kisera kwa kuzipatia majibu chanya changamoto zote .CCM iko tayari  wakati wowote  kumaliza utata  wowote  kwa njia ya majadiliano na mazungumzo mezani "Aliahidi 

Alimtaja Mwenyekiti  wa CCM  Rais Dk Samia  Suluhu  Hassan  ni Kiongozi  shupavu, Msikivu, Muungwana , anayeshaurika hivyo yuko tayari wakati  wowote  kushughulikia matatizo   kwa njia za kistaarabu. 

Katibu huyo Mwenezi   aliwataka Watanzania  kusoma mienendo  hatayarishi iliozikumba na inayoendelea kuzitatiza baadhi ya nchi, ambapo mizozo yake   imeacha vita ,mapigano na machafuko yasiokwisha.

"Watanzania tukatae ghiliba na ushawishi  utakaovuruga Amani na utulivu. Tuwe tayari  kujadili changamoto  kwa njia za wazi bila kuvutana mashati . Thamàni ya Amani , Umoja na Utulivu haiuzwi mahali popote Duniani "Alisema  Mbeto

Post a Comment

0 Comments