Na Alfan Mlacha-NIDA
Mamlaka ya Vitambalisho vya Taifa (NIDA) imeelekezwa kujidhatiti na kuongeza umakini katika uchakataji na utunzaji wa taarifa za watu ili kufanikisha mapinduzi ya uchumi wa kidijitali. Maelekezo hayo yametolewa na Mhe. George Simbachawene (Mb), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alipotembelea ofisi ya NIDA Makao Makuu - Dar es Salaam hivi karibuni.
‘’NIDA ni taasisi muhimu katika mapinduzi ya uchumi wa kidijitali ambayo yanategemea taarifa zenye usahihi na uhakika katika kupangilia uchumi wa nchi’’ alisema waziri.
Amesisitiza kuwa NIDA imepewa dhamana kubwa ya kuwa taasisi inayojishugulisha na Usajili na Utambuzi wa Watu wote wanaoishi nchini na kutunza taaarifa zao zikiwa sahihi na salama wakati wote.
Aidha, amefurahishwa na ubunifu wa NIDA kwenye Kitambulisho cha Taifa ambacho kinaweza kuwa kibebeo cha fedha pamoja na kuunganisha taasisi nyingine 137 ambazo zinaweza kutumia taarifa za NIDA katika kurahisisha huduma ya utambulisho kwa wananchi wanapoenda kupata huduma kwenye taasisi hizo.
Amewataka wananchi kutoa taarifa sahihi wakati wanapojisajili NIDA ili kujiepusha na marekebisho ya taarifa ya mara kwa mara ambayo hayana ulazima.
Usahihi wa taarifa ni suala muhimu katika utunzaji na uhifadhi kanzi data madhubuti ambayo inasaidia wananchi kupata huduma muhimu za kiuchumi na kijamii kama kufungua akaunti za kibenki, kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha, kufungua kampuni, matibabu, kujiunga na elimu katika ngazi mbalimbali, ajira na nyinginezo nyingi.
NIDA ina ofisi 154 katika wilaya zote nchi nzima na inaendelea kuongeza wigo wa kuwasajili wananchi kwa kuwafuata kwenye Kata na Vijiji wanakoishi kwa kuendesha mazoezi maalum ya usajili.
0 Comments