NA ABRAHAM NTAMBARA, LONGIDO
Halmashauri
ya Wilaya ya Longido leo, Desemba 11, 2025, imetoa mikopo ya asilimia 10 yenye
thamani ya shilingi 150,000,000
kwa jumla ya vikundi 26 vya
Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.
Akizungumza
katika hafla ya utoaji wa mikopo hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa J.K
Nyerere, Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe.
Kalli ameeleza mgawanyo wa mikopo hiyo kama ifuatavyo: Wanawake–Vikundi 11, shilingi milioni
60, Vijana–Vikundi 10, shilingi
milioni 62 na Watu Wenye Ulemavu–Vikundi
5, shilingi milioni 28
Mhe.
Kalli amevitaka vikundi hivyo kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa
ili kujiendeleza kiuchumi na siyo kwa matumizi ya starehe.
“Haya yanayofanyika leo ni maelekezo ya Mheshimiwa
Rais Samia Suluhu Hassan kwa Halmashauri zote nchini kukusanya na kutenga
asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya Wanawake,
Vijana na Makundi Maalum,” amesema
Mhe. Kalli na kuongeza,
“Baada ya kupata fedha hizi, nendeni mkazitumie
kwenye malengo yenu ili zizae, mrejeshe na wengine wapate. Tunaamini mtazitumia
vizuri na tutajionea matokeo.”
Amefafanua
kuwa mikopo hiyo ni ya awamu ya kwanza
kwa mwaka wa fedha 2025/2026, na kurejeshwa kwake kutasaidia kutoa
mikopo kwa vikundi vingine. Aliwataka wanufaika kuwa waaminifu na kurejesha
mikopo kwa wakati bila kufuatiliwa.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido Mhe. Thomas Ngobei amesema mikopo hiyo
imetokana na ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri. Ameahidi kuendelea
kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kuongeza kiwango cha mikopo kitakachotolewa
katika awamu zinazofuata.
Ameongeza
kuwa vikundi vilivyopata mikopo siyo kwamba ndivyo pekee vilivyoomba, na
amevitaka kuwa mabalozi wa kuhamasisha vikundi vingine kuendelea kuomba na kuwa
na imani na Halmashauri.
Naye
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe.
Peter Lekanet amewahimiza wanufaika kutumia fedha hizo kwa umakini na
kuonesha matokeo chanya ili Serikali iendelee kutenga fedha zaidi kwa ajili ya
mikopo ya wananchi.
Aidha,
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Longido Bi. Grace Mghase amesema kuwa kupitia mfumo mpya wa utoaji mikopo
ulioanzishwa na Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya shilingi 396,000,000 ilitolewa kwa vikundi 43
vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.
Kwa
mwaka huu wa fedha 2025/2026, Halmashauri imetoa shilingi 150,000,000 kwa vikundi 26, hivyo
kufanya jumla ya mikopo iliyotolewa kwa kipindi cha 2024/2025 hadi 2025/2026
kufikia shilingi 546,000,000.
Bi.
Mghase ameongeza kuwa vikundi vilivyonufaika vimekidhi vigezo baada ya
kufanyiwa tathmini na Kamati ya Mikopo ya Halmashauri, kupitishwa na Timu ya
Uendeshaji, na baadaye kuhakikiwa na Kamati ya Uhakiki ya Wilaya.
0 Comments