Na Mwandishi wetu
Baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki nchini wamejitokeza hadharani kukosoa na kufafanua matamshi yaliyotolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Askofu Jude Ruwa’ichi, wakidai kuwa kauli hizo zilikuwa na mwelekeo wa kisiasa na hukumu dhidi ya waumini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 27, 2025, muumini wa Kanisa Katoliki kutoka Parokia ya Mtakatifu Birigita Kongowe, Bw. Mackdeo Shilinde, alisema kuwa matamshi yaliyotamkwa na Askofu Mkuu akiwa madhabahuni yamekiuka maadili ya uongozi wa kiroho na kuacha athari kubwa za kisaikolojia na kiimani kwa waumini.
Bw. Shilinde ametaja matumizi ya maneno makali kama “lofa,” “mpumbavu,” “njaa njaa,” “msaliti,” na “ndumi la kuwili” kuwa hayana nafasi katika mahubiri ya Kikristo, akisema lugha hiyo imebeba hukumu nzito za maadili na dhamira ambazo hazilingani na misingi ya Injili.
Amesisitiza kuwa Kanisa linapaswa kuongozwa na mafundisho ya Biblia yanayokataza wanadamu kuhukumiana, akieleza kuwa hukumu ya haki ni ya Mungu pekee. Kwa mujibu wake, viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri kwa upendo, haki na dhamira safi, bila kutumia lugha inayoweza kuleta mgawanyiko miongoni mwa waumini.
Aidha, Bw. Shilinde ameonya juu ya hatari ya kuhamishia migogoro ya kijamii na kisiasa kwenye mimbari, akieleza kuwa mafundisho ya Kikristo yanahimiza maridhiano, msamaha na upatanisho badala ya migongano ya hadharani.
“Padri, Askofu na viongozi wengine wa Kanisa ni watumishi wa waumini. Kanisa ni jumuiya ya waamini wote, si taasisi ya watu wachache. Viongozi wa dini wanapaswa kuwa mfano wa unyenyekevu, utii wa Injili na maadili mema,” amesema Shilinde.
Vilevile, amesisitiza kuwa imani ya Kikristo haipaswi kutumika kama chombo cha kisiasa, akisema kuwa ingawa waumini ni raia wa Tanzania, imani yao inapaswa kubaki huru dhidi ya misukumo ya kisiasa. “Imani sio utaifa,” aliongeza.
Kwa pamoja, waumini hao wametoa wito wa kudumisha umoja, mshikamano na amani ndani ya Kanisa, huku wakiwahimiza viongozi wa dini kurejea kwenye kiini cha Injili kinachosisitiza upendo, haki, msamaha na amani.

0 Comments