DC LONGIDO ATOA SIKU 12 KWA VIKUNDI VINAVYODAIWA MIKOPO YA HALMASHAURI KUREJESHA







NA ABRAHAM NTAMBARA, LONGID

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, ametoa siku 12 kwa vikundi vinavyodaiwa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri vilivyokopa kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 kuhakikisha vinarejesha mikopo hiyo.

Kauli hiyo ameitoa leo Januari 19, 2026, wakati akizungumza na vikundi hivyo katika ukumbi wa Halmashauri wa JK Nyerere, ambapo amesema muda huo utaisha Januari 31, 2026.

Mhe. Kalli amesema kuanzia Februari 1, 2026, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa kushirikiana na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii watapita kikundi kwa kikundi kuhakiki kiasi kilichokopwa na kilichorejeshwa.

Amesisitiza kuwa vikundi ambavyo havitakuwa vimerejesha mikopo hiyo vitachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Lengo la kuwakopesha ni kuwasaidia mfanye maendeleo yenu, lakini ni lazima mrejeshe ili na wengine wapate. Mikopo hii inasaidia wananchi kuepuka mikopo ya kausha damu. Sasa kama mnakopeshwa na hamrejeshi, wengine watakopeshwa nini?” amesema Mhe. Kalli.

Hata hivyo, Mhe. Kalli amevitaka vikundi hivyo kutumia mikopo waliyopewa kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kugawana fedha hizo kwa matumizi binafsi yasiyohusiana na shughuli za kikundi, jambo ambalo limekuwa chanzo cha kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kalli amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kuwaandikia barua Watendaji wa Kata ili kuwapa maelekezo ya kuwafahamisha Waheshimiwa Madiwani kuwa wao wasiwe sababu ya vikundi vilivyokopeshwa kuacha kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Halmashauri hiyo, Bi. Rahma Kondo, amesema hakuna kikundi kitakachosamehewa kurejesha mikopo hiyo, na kuvitaka vikundi kuacha kutoa visingizio vya kushindwa kurejesha mikopo kwa madai ya ukame, akieleza kuwa baadhi ya vikundi vilikopa wakati hakukuwa na ukame.

Amebainisha kuwa kuna vikundi vinavyoendesha biashara kubwa na zinazoonekana wazi, lakini kwa makusudi vinashindwa kurejesha mikopo hiyo. Pia amewataka watumishi wa umma waliokopa kurejesha mikopo yao kwa kuwa orodha yao ipo.

Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri haina riba na hutolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments