NA ABRAHAM NTAMBARA, LONGIDO
Mkuu
wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, amewataka watumishi wa sekta ya afya
wilayani humo kuwa na lugha ya staha na kuwahudumia wagonjwa kwa heshima na
upendo wanapotoa huduma za afya.
DC
Kalli ametoa kauli hiyo leo Januari 9, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi
wa Kata ya Namanga baada ya kupokea malalamiko yao kuhusu baadhi ya watumishi
wa afya kutokuwa na lugha nzuri wanapowahudumia wagonjwa.
Kauli
hiyo imetolewa katika mwendelezo wa ziara yake ya Kata kwa Kata yenye lengo la
kusikiliza na kutatua kero za wananchi, sambamba na kuwahamasisha kujiunga na
Bima ya Afya kwa Wote.
“Kuanzia leo, mtumishi wa afya anayeshindwa
kuwahudumia wananchi ipasavyo aandike barua ya kuacha kazi. Mtumishi yeyote
mwenye lugha chafu hatumtaki,” amesema DC
Kalli.
Mhe.
Kalli ametoa rai kwa watumishi wa afya kuhakikisha wanawahudumia wananchi kwa
upendo na weledi, huku akisisitiza kuwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya
wilayani Longido vinapaswa kufanya kazi kwa masaa 24, na wagonjwa wasikose
huduma kutokana na watumishi kutokuwepo vituoni.
Aidha,
ametumia fursa hiyo kumwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Longido, Dkt. Mathew
Majani, kuhakikisha anawafikishia maelekezo hayo watumishi wote wa afya
wilayani humo.
Kwa
upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Majani, amepokea malalamiko hayo na
kuahidi kuyafanyia kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zenye
ubora wanaostahili.
Katika
hatua nyingine, DC Kalli amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada kubwa
kutatua changamoto ya upungufu wa maji katika Kata ya Namanga.
Ameeleza
kuwa mradi mkubwa wa maji wa Sinya unaendelea kutekelezwa na mkandarasi, na
kwamba ndani ya miezi minne mradi huo unatarajiwa kukamilika.
Amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha Namanga kupata maji ya kutosha na ya uhakika kwa matumizi ya wananchi.
0 Comments