BRELA YAWAKUMBUSHA WAJASIRIAMALI NCHINI KURASIMISHA BIASHARA ZAO.


Na Mwandishi Wetu 

Wakala wa Usajili wa Biashara la Leseni (BRELA) imewataka wajasiriamali wa bidhaa mbalimbali za viwanda kurasimisha biashara zao ili kuendelea kunufaika na fursa mbalimbali za kibiashara zinazopatikana nchini na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa tarehe 27 Februari ,2026 na Msaidizi wa Usajili Mkuu kutoka BRELA Bi. Hellen Mhina wakati akizungumzia ushiriki wa Wakala kwenye Maonyesho ya sita (6) ya Bidhaa za Viwanda na Biashara za Wanawake Tanzania yanayofanyika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika maonyesho hayo, Bi. Mhina alisema BRELA imesogeza huduma za papo kwa papo katika viwanja hivyo kwa lengo la kuwasaidia wajasiriamali wa biadhaa za viwanda pamoja na wananchi kwa ujumla wake kuzifikia huduma za BRELA. 

“Tunashiriki maonyesho haya kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi na wafanyabiashara wenye changamoto za kimfumo ili waweze kutatuliwa changamoto zao, tunatoa pia elimu juu ya Umiliki Manufaa kwa wamiliki wa kampuni lengo ni kuwaongezea uelewa zaidi hivyo tunawakaribisha sana,” alisema Bi. Mhina. 

Kwa upande wake Bw. Kassim Seif ambaye ni mfanyabiashara aliyepata huduma za papo kwa papo na kukabidhiwa cheti cha usajili wa Jina la Biashara kwenye banda la BRELA, alisema amepata msukumo wa kufanya biashara rasmi ili aweze kunufaika na fursa za kibiashara na kuitangaza zaidi biashara yake. 

“Watu tujitokeze kusajili majina ya biashara ili tufanye biashara kwa uwazi zaidi na kuweza kufikiwa na wateja wengi kwa sababu unavyosajili jina la biashara unakuwa unafahamika zaidi na watu wengi na unakuwa hauogopi kuitangaza ili kuvutia wateja wengi kwa sababu inakuwa rasmi,” alisisitiza Bw. Seif.

Huduma zinazotolewa na BRELA katika Maonyesho hayo ni pamoja na Usajili wa Jina la Biashara, Usajili wa Kampuni, Utoaji wa Leseni ya Biashara Kundi A na Leseni ya Kiwanda, Usajili wa Alama ya Biadhaa au Huduma pamoja na Utoaji wa Elimu ya Umiliki Manufaa kwa wamiliki wa Kampuni. 

Maonyesho ya Sita ya Bidhaa za Viwanda na Biashara za Wanawake Tanzania yanakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) ambapo BRELA inashiriki ili kuendeleza mkakati wake wa kusogeza huduma karibu kwa wananchi na kutoa elimu ya urasimishaji wa Biashara.

Post a Comment

0 Comments