MAAFISA 659 TCTA WAJENGEWA UWEZO KUHUSU URASIMISHAJI WA BIASHARA




NA MWANDISHI WETU 

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeendelea kuimarisha juhudi za kuhamasisha urasimishaji wa biashara kwa kutoa mafunzo maalum kwa wanafunzi Maafisa wa Magereza wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA), ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo wa kiuchumi mapema wakiwa bado kazini.

Mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, ambaye alieleza kuwa lengo kuu ni kuwajengea maafisa hao uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa kuanzisha na kurasimisha biashara zao kwa mujibu wa sheria. Alisisitiza kuwa urasimishaji wa biashara si tu unaleta uhalali wa kisheria, bali pia unafungua milango ya fursa mbalimbali za kifedha ikiwemo kupata tender mbalimbali.

“Ni muhimu kwa watumishi kuanza mapema kuwekeza na kurasimisha shughuli zako kabla ya kustaafu, ili kujenga msingi imara wa maisha ya baadaye,” alisisitiza Bw. Nyaisa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha TCTA, SACP. Willingtone Kahumuza, alisema mafunzo hayo yanaendana na kozi ya uongozi wanayosoma maafisa hao, akibainisha kuwa uongozi bora unapaswa kuambatana na uwezo wa kubuni, kuanzisha na kusimamia miradi ya uwekezaji. Alieleza kuwa jumla ya wanafunzi 659 wanapatiwa mafunzo hayo, hatua inayolenga kuwajengea uelewa mpana wa masuala ya kiuchumi na ujasiriamali.

Naye Mkuu wa Mafunzo Msaidizi, Inspekta Joseph Marwa, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za chuo kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kuwapa maafisa maarifa yatakayowasaidia sasa na baadaye. Aliongeza kuwa ushirikiano huo unaimarisha maandalizi ya maafisa kuwa viongozi wenye mtazamo mpana wa maendeleo binafsi na kitaasisi.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru BRELA kwa kuwapatia elimu hiyo muhimu. Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bi. Rhima Mohamed alisema mafunzo hayo yamewapa hamasa na ujasiri wa kuanza kujitegemea kwa kuanzisha biashara zitakazowaongezea kipato cha ziada.

BRELA imeahidi kuendelea kutoa mafunzo ya urasimishaji wa biashara kwa wadau mbalimbali nchini, ikiwa ni mkakati wa kuimarisha uchumi rasmi na kuwajengea wananchi utamaduni wa kufanya biashara kwa kufuata taratibu za kisheria.

Post a Comment

0 Comments