Dodoma
Utekelezaji wa miradi ya Uwekezaji na Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public-Private Partnership – PPP) unaendelea kupewa kipaumbele na Serikali, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa kwa weledi wa kisheria na kulinda maslahi ya taifa.
Hatua hiyo imejidhihirisha Februari 6, 2026 jijini Dodoma, wakati Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel M. Maneno, alipofunga rasmi mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali kuhusu usimamizi, uendeshaji na utekelezaji wa miradi ya PPP.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wakufunzi kutoka kampuni ya Cybiant ya nchini Malaysia, yamelenga kuongeza uwezo wa kitaalamu kwa Mawakili wa Serikali katika kusimamia mikataba ya miradi ya PPP, hususan miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Maneno amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea Mawakili wa Serikali ujuzi wa kisasa katika mbinu za majadiliano, uchambuzi wa mikataba, taratibu za ununuzi na utiaji saini wa mikataba, pamoja na usimamizi wa mikataba hiyo ili kuhakikisha miradi ya PPP inaleta tija kwa taifa.
Ameeleza kuwa ufanisi wa miradi ya PPP unategemea kwa kiwango kikubwa uwepo wa Mawakili wenye uelewa wa kina wa masuala ya kisheria, ili kuhakikisha mikataba inaandaliwa kwa misingi ya uwazi, uwajibikaji na kulinda rasilimali za nchi.
“Miradi ya PPP inahitaji Mawakili wenye weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha maslahi ya taifa yanalindwa kikamilifu,” amesema Maneno.
Aidha, amesisitiza kuwa uimarishaji wa uwezo wa Mawakili wa Serikali katika miradi ya PPP ni sehemu ya maandalizi ya kitaasisi kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Kupitia mafunzo haya, Serikali inalenga kupata Mawakili wenye ubora mkubwa katika kuandaa na kusimamia mikataba ya miradi mikubwa itakayosaidia kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji na kuchangia utekelezaji wa Dira 2050,” ameongeza.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Ildephonce Mukandara, kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, ameushukuru uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwezesha mafunzo hayo, akisema yamewawezesha kuongeza ujuzi katika upekuzi na usimamizi wa mikataba ya PPP, hatua itakayosaidia Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati endelevu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kuimarisha uwezo wa kisheria wa watumishi wake ili kuhakikisha utekelezaji thabiti wa miradi ya PPP nchini.


0 Comments