NA MWANDISHI WETU, LONGIDO
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, amesema Serikali imedhamiria kujenga soko la kisasa katika eneo la Namanga kuanzia mwaka wa fedha 2026/2027.
DC Kalli amebainisha hayo leo Februari 19, 2026 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Namanga wakati wa ziara ya kusikiliza kero zao. Amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya kufanya biashara mpakani mara soko hilo litakapokamilika.
“Tunataka kujenga soko la ghorofa hapa Namanga kuanzia bajeti ya mwaka wa fedha ujao kuanzia Julai. Tunataka kujenga soko la kisasa, kutakuwa na sehemu ya chakula, sehemu ya kuuza bidhaa, lakini pia kutakuwa na sehemu ya kina mama kunyonyeshea watoto wao,” amesema DC Kalli.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi wa Namanga kuendelea kulinda utulivu uliopo ili Serikali iendelee kuwaletea miradi ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa uchumi wao.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Namanga, Mhe. Baraka Solomon Mollel, amesema tayari amewasilisha ombi la shilingi bilioni moja katika Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Ujenzi na Miundombinu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa soko hilo.
Ameeleza kuwa wananchi wanaofanya biashara katika eneo litakalojengwa soko hilo watahamishwa kwa utaratibu maalumu, na pindi soko litakapokamilika watapewa kipaumbele cha kupatiwa maeneo ya kufanyia biashara ndani ya soko hilo.
Mhe. Mollel ameongeza kuwa soko hilo litakuwa na hadhi ya kimataifa na linatarajiwa kuhudumia pia wafanyabiashara kutoka nchi jirani.
0 Comments