SERIKALI YAIMARISHA USALAMA WA WANANCHI WA KARATU DHIDI YA MANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU




Na Saidi Lufune, Dodoma

Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vya askari wa wanyamapori na matumizi ya ndege nyuki kuimarisha doria katika makazi ya watu na maeneo ya hifadhi ili kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kuingia kwenye makazi ya wananchi

Hayo yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), katika kikao cha 6 cha Mkutano wa Pili wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la Mhe. Cecilia Daniel Paresso (Mb), aliyetaka kufahamu juu ya mkakati wa Serikali katika kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu wanaotoka katika Hifadhi ya Ngorongoro na Ziwa Manyara

Mhe. Chande amefafanua kuwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Askari katika Kijiji cha Lostete kilichopo mpakani mwa hifadhi, na kutumia Askari wa Vijiji (VGS) wanaoshirikiana na askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, Serikali inatarajia kujenga uzio wa umeme wenye urefu wa kilometa 15 ili kukinga na kuzuia tembo na wanyamapori wengine kuingia kwenye makazi ya wananchi.

“Serikali imeandaa Mkakati mpya wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wa miaka kumi kuanzia 2025/26 hadi 2035/36. Mkakati huu utatekelezwa kwa ushirikiano na wizara za kisekta ikiwemo OWM-TAMISEMI, Maliasili na Utalii, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha kuwa jitihada za kupunguza changamoto hii zinafanyika kwa pamoja na kwa ufanisi.” Aliongeza Mhe. Chande

Post a Comment

0 Comments