Na Saidi Lufune, Morogoro
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imetakiwa kuongeza nguvu katika upandaji miti, uzalishaji na usafirisha nje ya nchi kufikia tani 50 kwa mwaka tofauti na sasa ambapo tani elf 9 tu ndio husafirishwa kwa mwaka.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb.) ameyasema hayo leo Mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 4 wa mwaka wa TFS na kusisitiza juu ya kuelimisha jamii kuhusu ufugaji bora wa nyuki ili jamii iendelee kujiingizia kipato kwa kujiajiri kupitia mazao yatokanayo na misitu.
Pia amepongeza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu na kutatua migogoro ya mipaka kati ya maeneo ya hifadhi na vijiji kwa asilimia kubwa.
Aidha, amesisitiza juu ya kuwa waaminifu katika kazi zao; subira na ustahimilivu; pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia dhana ya utu ikiwa ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwatumikia watanzania
Mhe. Chande ameielekeza TFS kujiimarisha katika kubuni mazao mapya ya utalii yatokanayo na rasilimali za misitu ili kuvutia watalii wengi zaidi kwenye maeneo yao na hatimaye kuchagiza kutimiza lengo la Serikali la kufikisha idadi ya watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bw. Bernard Patrice Marcelline amesisitiza Menejiment ya TFS juu ya umuhimu wa kuoanisha mipango ya TFS na Ilani ya Uchaguzi 2025–2030 pamoja na ahadi za bajeti ya 2025/26; Mpango Mkakati wa Nne (2026/27–2030/31); sambamba na kuzingatia maslahi ya watumishi katika maandalizi ya bajeti yam waka 2026/2027.
Awali Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo amesema kuwa licha ya uwepo wa changamoto nyingi za uhifadhi TFS inaendelea na jitihada mbalimbali za kulinda misitu ikiwemo Matumizi ya taknelojia ya TEHAMA; kutoa mafunzo kwa wananchi juu ya upandaji miti na uhifadhi wa Misitu; kuweka Sheria ndogo ndogo dhidi ya uharibifu wa Misitu sambamba na mkakati wa miaka thelathini wa usimamizi wa mashamba ya misitu kutoka hekta 510,663 mwaka 2020/2021 hadi hekta 588,555 mwaka 2024/2025
0 Comments