*Watembelea mradi kuona ufanisi wake
*Shilingi bilioni 118 zatumika kutekeleza mradi
*Watoa rai awamu ya pili kuanza kwa kasi
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa Mradi wa Uzalishaji Umeme kwa nguvu ya Jua wa Kishapu wenye uwezo wa Megawati 50 unaotekelezwa katika Mkoa wa Shinyanga.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Subira Mgallu, mara baada ya Kamati kutembelea mradi huo tarehe 13 Machi, 2026 kwa lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji wake pamoja na ufanisi wa matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mhe. Mgallu alisema mradi huo ni hatua muhimu katika mageuzi ya sekta ya nishati nchini kutokana na matumizi ya teknolojia ya nishati jadidifu.
“Tumetembelea mradi huu wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia teknolojia ya jua na tunaona ni mapinduzi makubwa katika sekta ya nishati nchini. Hii ni hatua muhimu kwani kwa mara ya kwanza Tanzania inapata Megawati 50 za umeme kutoka kwenye nishati ya jua,” alisema Mhe. Mgallu.
Alisema Kamati imeridhishwa na namna fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo zimetumika ipasavyo na kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi.
“Kama Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, tumeridhishwa na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya mradi huu. Tunaona wazi kuwa fedha hizo zimetumika vizuri katika utekelezaji wa mradi huu wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 118,” alieleza.
Aidha, alisema mradi huo tayari umeanza kuchangia Megawati 50 katika Mfumo wa Gridi ya Taifa, hatua inayochangia kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini pamoja na kuimarisha vyanzo mseto vya nishati.
“Utekelezaji wa mradi huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kunakuwa na vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme. Hii inaongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati ya umeme nchini,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, alisema mradi wa Kishapu unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ya Megawati 50 tayari imekamilika na imeanza kuingiza umeme katika Gridi ya Taifa.
“Mradi huu una awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ya Megawati 50 tayari imekamilika na imeanza kuingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa. Awamu ya pili itahusisha uzalishaji wa Megawati 100 zaidi na kufanya jumla ya Megawati 150 kutoka katika mradi huu,” alisema Mhe. Ndejembi.
Kamati hiyo imetoa Rai kwa Wizara ya Nishati na TANESCO inaendelea kuendelea na mikakati ya kuanza utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo ili kuongeza zaidi uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini.


.jpeg)

0 Comments