Shule ya sekondari Makongo imeibuka mshindi wa kwanza kitaifa katika mradi wa mashindano ya kwanza ya Klabu za shule za Sekondari katika eneo la Miliki Ubunifu (IP School Club Project), yaliyofanyika leo tarehe 6 Marchi, 2026 jijini Dar es Salaam.
Awali akifungua mashindano hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Bw. Moses Liota ambae amemuwakilisha Dkt. Aneth Komba amesema kuwa, BRELA na COSOTA wanatakiwa kuhakikisha mashindano hayo yanabeba sura ya kitaifa ili kujenga uchumi wa nchi.
“Serikali imeamua kujikita katika kujenga uchumi wa nchi kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa za kujiajiri, hivyo BRELA na COSOTA mnatakiwa kushirikiana katika kutoa taarifa kwa wadau kuhusu miliki ubunifu,’’ alisema Liota.
Mashindano hayo kwa shule za Sekondari kuhusu miliki bunifu yamehusisha shule tano kutoka mikoa minne ambapo mshindi wa pili ni shule ya sekondari Kiembe samaki kutoka Zanzibar, mshindi wa tatu ni shule ya sekondari Sikirari ya Kilimanjaro.
Mshindi wa kwanza ambaye ni Shule ya Sekondari Makongo itaiwakilisha nchi katika mashindano ya Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO).
Shule nyingine zilizoshiriki ni pamoja na shule ya Ufundi Tanga Technical na St. Joseph Cathedral ya jijini Dar es Salaam.
Awali akizungumza katika mashindano hayo Kaimu Mtendaji Mkuu wa COSOTA Bw. Philemon Kilaka amesema kuwa mashindano hayo yanafanyika baada ya kukamilishwa hatua tatu ambazo ni mafunzo kwa walimu na wanafunzi, mashindano ya kitaifa na mashindano ya kimataifa.
Mashindano hayo yalihusisha uwasilishaji wa ubunifu ambao umefanywa, kujibu maswali yaliyoulizwa ambapo shule ya Sekondari Makongo ili tengeneza igizo linalo elezea jinsi msanii anavyoibiwa kazi ya sanaa kwa kuto kujua hatua za kufuata ili kulinda haki miliki zake ili kuweza kunufaika na kazi ya ubunifu wake; sambamba na kujibu maswali kwa ufasaa na kujiamini kwa kile wanachokifanya.
Mradi wa mashindano ya kwanza ya Klabu za shule za Sekondari katika eneo la Miliki Ubunifu nchini yamefanyika chini ya usimamizi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na leseni (BRELA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA).
Mradi huo umeanza kutekelezwa nchini mwaka 2025 ukiratibiwa na Shirika la Miliki Bunifu Afrika (ARIPO) kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) kwa ufadhili wa Wizara ya Utamaduni, Michezo, na Utalii ya Korea.



0 Comments