TARURA yajenga barabara za lami kuboresha miundombinu Karatu, waendesha bodaboda watakiwa kupunguza mwendo



*Wananchi wasema miradi imeongeza biashara na kurahisisha usafiri

Na Mwandishi Wetu, Karatu

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Karatu umeendelea kuboresha miundombinu ya barabara kwa kujenga barabara za lami ndani ya mji huo, hatua inayolenga kurahisisha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Hata hivyo, waendesha bodaboda wametakiwa kupunguza mwendo kufuatia kuimarika kwa barabara hizo ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo au majeraha.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA wilaya ya Karatu Mhandisi Msetu Madara wakati akiongea na waandishi wa habari wilayani hapo.

Mhandisi Madara amesema kuwa TARURA wilaya ya Karatu inahudumia jumla ya kilometa 771 za barabara, ambapo barabara za lami kilometa 4.34 zilizopo katika Mji Mdogo wa Karatu, barabara za changarawe Km. 315.816 na udongo ni Km. 451.400.

Aidha, amesema Wakala huo unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara mpya za lami ndani ya mji huo.

Ameongeza kusema kwamba wanajitahidi kuhakikisha barabara za Karatu zinaboreshwa ili zipitike majira yote ya mwaka.

“Tunajitahidi kuhakikisha barabara za Karatu zinakuwa nzuri na zinapitika majira yote ya mwaka. Wilaya ya Karatu ni mji wa kitalii unaopokea watalii wengi wanaotembelea vivutio vya utalii kama Hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti, hivyo mkakati wetu ni kuhakikisha mji wote unakuwa na barabara za lami”, alisema.

Aliongeza kuwa katika ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilometa 1.4 ambazo zimejengwa hivi karibuni zimejengwa mitaro ya maji katika pande zote mbili za barabara hizo ili kulinda miundombinu dhidi ya uharibifu. Pia kuna mpango wa kuweka taa za barabarani katika barabara mpya ili kuimarisha usalama wa watumiaji wakati wa usiku na kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika hadi nyakati za usiku.

Aidha, aliongeza kuwa hivi sasa wamekamilisha ujenzi wa daraja la mawe la Chemchem lililopo katika Kijiji cha Chemchem lenye urefu wa mita 21 na upana wa mita 7. Ujenzi huo unaambatana na barabara yenye urefu wa Km. 5 inayounganisha vijiji vya Endallah, Manusai, Masabeda, Endamarariek, Basodawishi, Chemchem, Kilimamoja, Gidibaso, Getamock, Qaru na Endabash.

Aliongeza kuwa hadi Februari mwaka huu, TARURA imefanikiwa kujenga madaraja sita(6) ili kuondoa vikwazo vya usafiri na kurahisisha wananchi kupata huduma za kijamii.

Hata hivyo, TARURA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi, hususan vijana wanaoendesha pikipiki, kuendesha kwa mwendo unaozingatia usalama barabarani ili kuepuka ajali. Alisisitiza kuwa vijana hao wanapaswa kutambua kuwa wao ni nguvu kazi ya Taifa na wanapaswa kujilinda.

Naye, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mjini Kati, Ndugu Elisifa Amma, alisema kabla ya ujenzi wa barabara hizo eneo hilo lilikuwa na barabara mbovu zilizokuwa na mashimo na matope hali iliyokuwa ikisababisha usumbufu kwa wananchi.

Alisema tangu kujengwa kwa barabara hizo, wananchi wamefurahia mabadiliko hayo na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu na kuufanya mji huo kuwa wa kisasa.

“Magari mengi sasa yanapita kwa urahisi yakileta watalii, hali ambayo imeongeza biashara. Hata fremu za maduka sasa zinapangishwa kwa urahisi kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi,” alisema.

Kwa upande wake, Bi. Salome Minja ambaye ni mjasiriamali wa mgahawa katika Mji wa Karatu, alisema awali ubovu wa barabara uliwakosesha wateja kutokana na matope wakati wa mvua na vumbi wakati wa kiangazi.

“Kwa sasa hali imebadilika mji umechangamka na biashara zinaendelea vizuri. Tunapata wateja wengi zaidi na kipato kimeongezeka,” alisema.

Msimamizi wa miradi hiyo, Mhandisi Daines Simba, alisema hapo awali mji wa Karatu haukuwa na barabara za lami lakini sasa wamefanikiwa kujenga miundombinu hiyo ambayo imechochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.

Alisema pia miradi hiyo imewezesha kuajiri vijana wengi katika kazi za ujenzi, hatua iliyosaidia kupunguza vitendo vya uhalifu na kuongeza kipato kwa wananchi.

Naye mkazi wa Chemchem, Philipines Samwuel, alisema kabla ya ujenzi wa daraja hilo wananchi na magari walikuwa wakipata shida kuvuka hasa kipindi cha masika.

Alisema kwa sasa wanaishukuru serikali kwa kukamilisha ujenzi wa daraja hilo kwani limewezesha shughuli za usafiri na usafirishaji kufanyika wakati wote wa mwaka.

Post a Comment

0 Comments