NA MWANDISHI WETU, LONGIDO
Baraza la Biashara Wilaya ya Longido limetakiwa kuwa daraja la kutangaza fursa zilizopo wilayani humo ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza.
Amesema Longido ni eneo muhimu katika shughuli za biashara kutokana na wingi wa fursa zilizopo, hususan katika sekta ya ufugaji na biashara ya kuvusha bidhaa kwenda nchi jirani.
“Longido ni eneo moja muhimu sana katika ufanyaji wa biashara. Fursa zilizopo hapa ni kubwa, ikiwemo uwekezaji katika biashara ya ufugaji na biashara ya kuvusha bidhaa kwenda nchi jirani,” amesema Mhe. Kalli.
Ameongeza kuwa Wilaya hiyo inaongoza kwa shughuli za ufugaji, huku kilimo kikifanyika kwa kiwango kidogo katika kata chache kama Kamwanga na Olmolog kati ya kata 20 zilizopo.
Amesema nchi jirani zinategemea kwa kiasi kikubwa mifugo kutoka Longido, jambo linaloonyesha umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa eneo hilo.
Aidha, ameeleza kuwa kupitia mikutano ya Baraza la Biashara,
wafanyabiashara hupata fursa ya kujifunza kuhusu huduma za kifedha kutoka kwa
taasisi za benki pamoja na kujulishwa sera na mifumo inayorahisisha biashara
zao.
“Wafugaji wanaweza kufanya ufugaji wa kibiashara kwa kunenepesha mifugo na kuiuza baada ya muda mfupi, hivyo kuongeza kipato kwa haraka,” alisisitiza.
Mhe. Kalli amebainisha pia kuwa sekta ya utalii ni miongoni mwa fursa muhimu zilizopo Longido, na ametoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza ili kukuza uchumi wa Wilaya hiyo.
Aidha, ameongeza kuwa kuna fursa katika uwekezaji wa viwanda vya ngozi, akieleza kuwa licha ya Longido kuwa na mifugo mingi, kiwanda cha ngozi kilichopo Himo mkoani Kilimanjaro kinanufaika na rasilimali hizo.
Amesisitiza umuhimu wa wafugaji kuboresha ubora wa ngozi kwa kuepuka kuweka alama nyingi kwenye mifugo, ili kuongeza thamani ya bidhaa hiyo sokoni.
“Kupitia ufugaji, mfugaji anaweza kunufaika kwa kupata nyama,
ngozi na bidhaa nyingine, hivyo kuongeza thamani ya mifugo yake,” amesema.



0 Comments