NA MWANDISHI WETU

Naibu Waziri wa Nishati,Mhe. Salome Makamba ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Misri, ambapo alipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Richard Makanzo.

Katika mazungumzo yao, Balozi Makanzo alieleza majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na ubalozi huo, pamoja na kuainisha fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, umeme, uchukuzi na biashara. 

Balozi Makanzo alieleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali za Tanzania na Misri katika sekta hizo unalenga kuwanufaisha wananchi na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Mhe. Salome alimpongeza Balozi Makanzo kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na timu yake, hususan katika kuendeleza mahusiano si tu kati ya Tanzania na Misri, bali pia na balozi za nchi nyingine zilizopo nchini humo.

Mhe. Salome yupo nchini Misri kwa ajili ya kushiriki mkutano wa East African Power Pool, utakaofanyika Aprili 29, 2026 jijini Cairo. 

Mkutano huo utajadili masuala muhimu ya sekta ya nishati miongoni mwa nchi wanachama, ikiwemo uunganishaji wa gridi za taifa na biashara ya umeme baina ya nchi hizo.

Mkutano huo umetanguliwa na vikao vya wataalamu kutoka sekta ya nishati katika nchi wanachama, vikilenga kuweka msingi wa majadiliano ya viongozi.