▪️Ni sehemu ya utatuzi wa mgogoro wa Kikundi cha Isunda na wamiliki wa mashamba na maduara
▪️Waziri Mavunde aelekeza kuwasilishwa kwa nyaraka muhimu ndani ya siku 3
▪️Aagiza shughuli za uchimbaji Busulwangili kusimama mpaka kukamilika kwa uchunguzi wa mchakato wa ubia
▪️Awataka wadau wa sekta ya madini kufuata sheria na taratibu zilizowekwa
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ametoa maelekezo ya haraka kutatua mgogoro kati ya Kikundi cha Isunda (wamiliki wa leseni), wamiliki wa mashamba na wamiliki wa maduara katika kijiji cha Busulwagili, wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga.
Maelekezo hayo yametolewa Aprili 14, 2026, katika ukumbi wa Tanzanite, Makao Makuu ya Madini, Dodoma, wakati wa kikao kilichowakutanisha wadau hao ili kusikiliza hoja na kupata suluhisho la uhalali wa umiliki na uzalishaji.
Amekiagiza Kikundi cha Isunda kusitisha mara moja shughuli zote za kuendelea na uchimbaji hadi wawasilishe muhtasari wa kikao utakaonesha makubaliano ya wazi kuhusu haki waliyopewa kwanza wenye maduara kuwekeza kabla mwekezaji mwingine kuendelea na uwekezaji kama ambavyo Kanuni ya 18A ya Haki Madini inavyoeleza.
Amefafanua kuwa Sheria ya Haki za Madini (kifungu 18A) inataka kama mwenye Leseni kaingiza wachimbaji wameweka maduara siku atakapopata mwekezaji mwingine awape kwanza haki ya kwanza ya uwekezaji wenye maduara na si vinginevyo.
"Leseni ni kwa shughuli za uchimbaji pekee, siyo upangishaji, ukiukwaji wa taratibu wowote hautavumiliwa" amesema Mhe. Mavunde
Ameongeza kuwa wamiliki wa leseni na maduara watalazimika kuingia mikataba rasmi ya ushirikiano kabla ya kuanza uchimbaji, ili kuzuia migogoro.
Hata hivyo, Waziri ameonya uongozi wa Kikundi kuacha kutoa taarifa zisizo sahihi zinazoleta taharuki kwa jamii inayopelekea migogoro kati ya wachimbaji wadogo na wamiliki wa leseni.
Aidha, ameielekeza Tume ya Madini Tanzania kutosaini mkataba wowote wa kiufundi hadi ijiridhishe, kuwa hakuna mgogoro kati ya wamiliki wote wa leseni na wachimbaji wa maduara
" Itapelekwa timu ya wataalamu katika kila duara kutathmini uzalishaji, mrabaha wa Serikali na kuhakikisha uwazi na uwajibikaji." amesema Mhe. Waziri
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa amesema kuwa ufumbuzi wa kudumu unategemea majadiliano ya uwazi yanayozingatia sheria, haki na maslahi ya pande zote.


0 Comments