BRELA KUONGEZA THAMANI YA MICHEZO NCHINI KUPITIA MILIKI UBUNIFU




NA MWANDISHI WETU

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imesema kuelekea Maadhimisho ya siku ya Miliki Ubunifu Duniani (IP Day), BRELA imedhamiria kukuza na kuongeza thamani zaidi ya michezo nchini kupitia haki za Miliki Ubunifu.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 05 Mei, 2026 na Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA Bi. Loy Mhando wakati akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa katika ufunguzi wa Warsha maalumu kwa wadau wa sekta ya michezo nchini.

Katika hotuba yake, Bi. Mhando alisema kuwa katika sekta ya michezo, Miliki Ubunifu ina nafasi ya kipekee na muhimu kwa kuwa, mbali na kuhusisha ushindani wa kimichezo, lakini pia sekta hiyo ina thamani kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla wake.

“Mara nyingi tumeshuhudia matumizi yasiyo halali ya Alama za timu na uuzaji wa bidhaa bandia jambo ambalo hupelekea upotevu wa mapato, hii inapunguza uwezo wa wadau wa michezo kunufaika na juhudi zao. Warsha hii inatoa elimu sahihi kuhusu Miliki Ubunifu na nafasi yake katika kukuza sekta ya michezo” alisema Bi. Loy Mhando.

Bi. Mhando alieleza pia ni muhimu kuelewa kuwa Miliki Ubunifu ni rasilimali yenye thamani kubwa kwenye uchumi inayohusisha haki za kisheria katika Alama za Biashara ha Huduma, Hakimiliki, Hataza, Maumbo Bunifu na Siri za Biashara ambapo haki hizo zinatoa ulinzi kwa wabunifu na wamiliki wa kazi za ubunifu na fursa zinazochochea ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mhandisi Leodgar Tenga aliwataka wadau wa michezo walioshiriki katika Warsha hiyo kutumia vizuri elimu ya Miliki Ubunifu kwa kuhakikisha Taifa linafaidika na mashindano ya AfCON yatakayofanyika hapa nchini mwaka 2027.

“Nitoe shukran kwa waandaaji wa Warsha hii kwani imekuja wakati muafaka ambao nchi yetu inaandaa mashindano makubwa ya AfCON, niwaombe Washiriki wote tukawe wanafunzi wazuri tukitoka hapa na tukayatumie vizuri Mafunzo haya” alisema Mhandisi Leodgar Tenga. 

Warsha ya Miliki Ubunifu kwa wadau wa michezo nchini imewakutanisha wadau wa michezo kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani ili kuhakikisha Sekta hiyo inaongezewa thamani ambapo Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kulinda na kuendeleza Miliki Ubunifu kupitia Taasisi mbalimbali ikiwemo BRELA.

Post a Comment

0 Comments