NA MWANDISHI WETU
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umepokea tuzo kwa kushika nafasi ya tatu miongoni mwa taasisi zinazochangia gawio kwa Serikali kwa wakati na kwa uendelevu kwa kipindi cha miaka saba mfululizo kuanzia mwaka 2019/2020 hadi mwaka 2025/2026.
Tuzo hiyo imetolewa leo tarehe 30 Juni, 2026 katika hafla ya utoaji wa gawio kwa Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema kuwa BRELA na taasisi nyingine zilizopo katika kundi hilo la tuzo zimeendelea kuchangia kwa wakati na kwa uendelevu, uthabiti na kwa kiasi stahiki huku zikijisukuma zenyewe kutimiza matakwa ya sheria na kuchangia kwa asilimia kama ilivyoelekezwa.
"Kundi hili tumeangalia taasisi zinazochangia kwa wakati na kwa uendelevu, Tasisi ambazo kwa kipindi chote zimekuwa zikichangia kwa uthabiti na kwa kiasi stahiki, BRELA kwa kipindi cha miaka saba wamekuwa wakichangia kiasi cha Tsh. Bilioni 15.6 kwa kila mwaka." alisema Bw. Nehemiah Mchechu.
Tuzo hiyo imepokelewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA Prof. Neema Mori. ambaye aliambatana Bw. Godfrey Nyaisa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa akizungumza na watumishi wa BRELA baada ya kupata tuzo hiyo aliwapongeza watumishi kwa kufanya kazi kwa bidii huku akiwasisitiza kuendelea kujituma na kufanya kazi kwa nidhamu na weledi ili kupata matunda yaliyo bora.
“Hii ni tuzo hii ni kwaajili ya wafanyakazi wote, mimi niwapongeze kwakuwa haya ni matokeo ya kufanya kazi kwa bidii, siku zote ukifanya kazi kwa bidii lazima utaona matunda yake na haya ni matunda bora ya kazi mliyoifanya.” Alisema Bw. Nyaisa
Aidha, katika hafla hiyo BRELA pia imekabidhi Serikali gawio la Tsh. Bilioni Kumi na Moja, Milioni Mia Nne Tisini na Nne, Laki Moja Kumi na Saba, Elfu Mia Saba Ishirini na Nane (Tsh. 11,494,117,728), ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuongeza mapato ya Serikali na kuunga mkono juhudi za maendeleo ya taifa.
.jpeg)

0 Comments