NGORONGORO YAWAVUTIA MAELFU SABASABA KWA MATUKIO YA UTALII MUBASHARA


NA MWANDISHI WETU

Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) limeendelea kuvutia maelfu ya wananchi kupitia matangazo ya moja kwa moja yanayoonesha vivutio vya utalii vya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Kupitia runinga kubwa iliyofungwa katika banda hilo, wageni wanapata fursa ya kushuhudia maajabu ya Kreta ya Ngorongoro, makundi ya wanyama mbalimbali wakiwemo pundamilia, nyumbu, swala, nyati, pamoja na wanyama adimu kama faru, simba, tembo na chui, hali inayowafanya wajisikie kana kwamba wapo ndani ya hifadhi hiyo.

Afisa Uhusiano Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bw. Walter Mairo, amesema kuwa teknolojia hiyo inawawezesha wageni kufuatilia matukio mbalimbali yanayotokea ndani ya hifadhi, ikiwemo maisha ya wanyama katika Kreta ya Ngorongoro na tambarare za Ndutu, ambako hushuhudiwa mzunguko wa maisha ya nyumbu kuanzia kuzaliwa, kukua, kuhama na kurejea kila mwaka kwa ajili ya kuanzisha kizazi kipya.

Ameongeza kuwa matangazo hayo ya mubashara yanaonesha jinsi teknolojia ya kidijitali na utalii wa asili vinavyoweza kushirikiana katika kuelimisha, kuburudisha na kuitangaza Ngorongoro duniani. Amesema Ngorongoro si hifadhi ya wanyamapori pekee, bali ni jukwaa la kimataifa linalounganisha urithi wa asili, biashara na teknolojia katika eneo moja.

Wananchi wanakaribishwa kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya Sabasaba ili kujionea vivutio hivyo na kupata simulizi mbalimbali kuhusu Ngorongoro. Timu ya wataalamu wa hifadhi hiyo ipo tayari kuwapa wageni taarifa na uzoefu unaoonesha kuwa Ngorongoro si mahali pa kutazama vivutio pekee, bali ni mahali pa kujifunza, kuelewa na kuishi uzoefu wa kipekee usiosahaulika.

 


Post a Comment

0 Comments