*Mfumo wa Smart house humwezesha mtumiaji kudhibiti vifaa vya umeme akiwa popote alipo

* Inatumia wiring za kisasa zinazoweza kuokoa nyumba na majanga ya moto sambamba na kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wananchi wanaotembelea Banda la TANESCO katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Saba Saba) wanaendelea kupata elimu kuhusu teknolojia ya Nyumba Janja (Smart House), inayorahisisha matumizi ya umeme kwa kumwezesha mtumiaji kudhibiti vifaa vya umeme akiwa popote alipo.

Kupitia mfumo wa kidijitali wa Smart Life, mtumiaji anaweza kuwasha na kuzima vifaa vya umeme kwa kutumia simu ya mkononi kupitia mtandao, hata akiwa mbali na nyumba yake. Teknolojia hiyo inalenga kuongeza urahisi, usalama na udhibiti katika matumizi ya umeme majumbani na maofisini.

Mbali na kudhibiti vifaa vya umeme kwa njia ya mtandao, mfumo huo humwezesha mtumiaji kufuatilia matumizi ya umeme ya kila siku na kubaini kifaa kinachotumia umeme mwingi zaidi, hatua inayosaidia kupanga matumizi bora ya nishati na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Aidha, mfumo wa Smart Life hutoa taarifa za hitilafu zinazoweza kujitokeza kwenye vifaa vya umeme vilivyounganishwa katika mfumo huo kupitia simu ya mkononi, hivyo kumwezesha mtumiaji kuchukua hatua kwa wakati.

Vilevile, mtumiaji anaweza kupanga muda wa kuwasha na kuzima vifaa vya umeme pamoja na kudhibiti matumizi ya soketi na swichi za umeme popote alipo, mradi awe na huduma ya intaneti.

Mfumo wa Smart Life unaweza kufungwa katika nyumba yenye mfumo wa kawaida wa umeme kwa kuunganisha vifaa maalumu vya Smart Socket na Smart Switch, vinavyowezesha mtumiaji kufurahia urahisi wa kudhibiti matumizi ya umeme kwa njia ya kidijitali.