WAWEKEZAJI KUTOKA CHINA WAVUTIWA NA FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA TASNIA YA MBOLEA






NA MWANDISHI WETU

Wawekezaji kutoka nchini China wametembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), ambapo wameonesha nia ya kuwekeza katika tasnia ya mbolea nchini kwa kuanzisha kiwanda cha kuchanganya mbolea (Blending Facility).

Akizungumza baada ya kupokea elimu katika banda la TFRA, mmoja wa wawekezaji hao, Bon Chen, amesema wamevutiwa na fursa zilizopo nchini pamoja na maelezo waliyopatiwa kuhusu taratibu za usajili wa wawekezaji na mbolea, hatua ambayo imewapa hamasa ya kuendelea na mchakato wa uwekezaji.

Amesema wataendelea kushirikiana na TFRA kwa kufanya mawasiliano ya karibu ili kukamilisha taratibu zote zinazohitajika kwa ajili ya kuanzisha kiwanda hicho, hatua itakayochangia kuongeza upatikanaji wa mbolea nchini.

Kwa upande wake, Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’ondya, amesema Mamlaka inaendelea kutoa elimu kuhusu fursa za uwekezaji katika tasnia ya mbolea pamoja na kusimamia taratibu za usajili wa wawekezaji na mbolea ili kuhakikisha uwekezaji unafanyika kwa kuzingatia sheria na viwango vinavyotakiwa.

Ameongeza kuwa TFRA itaendelea kuwahudumia wawekezaji kwa kuwapatia taarifa na mwongozo unaohitajika ili kuvutia uwekezaji zaidi katika tasnia ya mbolea na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

TFRA inaendelea kufungua fursa zilizopo kwenye tasnia ya mbolea kupitia monesho hayo, ambapo wafanyabiashara wa mbolea, wawekezaji, wakulima na wadau wa tasnia wanapata nafasi ya kuifikia Mamlaka hiyo kupitia maonesho ya sabasaba

Post a Comment

0 Comments