ZIWA NGOZI LAVUTA MAMIA SABASABA, WAGENI WASHANGAZWA NA “RAMANI YA AFRIKA” JUU YA MLIMA




Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wageni wanaotembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) wameendelea kuvutiwa na simulizi kuhusu Ziwa Ngozi, moja ya vivutio vya kipekee vya utalii nchini, kinachopatikana ndani ya Hifadhi ya Mazingira ya Msitu wa Mlima Rungwe mkoani Mbeya.

Mvuto huo umechangiwa na maelezo yanayotolewa na Afisa Utalii wa Hifadhi ya Mazingira ya Msitu wa Mlima Rungwe, Jesca Mgata (pichani) ambaye amekuwa akiwafafanulia wageni historia, maajabu na upekee wa ziwa hilo linalotajwa kuwa la pili kwa ukubwa miongoni mwa maziwa ya kreta barani Afrika.

Akiwa katika banda la TFS, Jesca Mgata amesema wengi wanaofika kushuhudia maonesho hushangazwa wanapoelezwa kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya vivutio vya utalii ambavyo bado havijafahamika vya kutosha, huku Ziwa Ngozi likiwa miongoni mwa vivutio vinavyozidi kupata umaarufu.

“Baadhi ya wageni hawaamini wanapoona picha za ziwa hili. Tunawaeleza kuwa liko juu ya mlima, limezungukwa na msitu mnene na limetokana na mlipuko wa volkano. Wengi huamua kulitembelea mara baada ya kupata taarifa hizi,” alisema.

Alieleza kuwa moja ya maajabu makubwa ya Ziwa Ngozi ni uwezo wake wa kuakisi umbo linalofanana na ramani ya Bara la Afrika, likiwa na mwonekano unaoonesha pande za kusini, mashariki, magharibi na kaskazini pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, jambo linalowavutia watafiti, wapiga picha na watalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Jesca Mgata, ziwa hilo linapatikana katika Milima ya Uporoto ndani ya Hifadhi ya Mazingira ya Msitu wa Mlima Rungwe na ni ziwa la kreta lililotokana na shughuli za volkano, tofauti na maziwa mengine makubwa ya asili. Ziwa hilo lina urefu wa takribani kilomita 2.5, upana wa kilomita 1.5, kina cha mita 74 na eneo la zaidi ya hekta 9,332.

Alisema mazingira ya ziwa hilo yanatoa fursa za utalii wa ikolojia, matembezi ya milimani, utazamaji wa ndege, upigaji picha na tafiti za kijiolojia, huku mandhari yake ya kipekee yakiendelea kuwavutia wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Mgata alibainisha kuwa TFS inaendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba kutangaza vivutio vilivyopo kwenye hifadhi za misitu ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na wa kimataifa, akisisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kujivunia na kutembelea hazina zao za asili.

Katika maonesho hayo, banda la TFS limeendelea kupokea maelfu ya wageni wanaojifunza kuhusu utalii wa misitu, uhifadhi wa mazingira na vivutio vya kipekee vinavyopatikana nchini, huku simulizi za Ziwa Ngozi zikizidi kuhamasisha wengi kupanga safari ya kutembelea Hifadhi ya Mazingira ya Msitu wa Mlima Rungwe.

Post a Comment

0 Comments