ASKARI WA TAWA WAMDHIBITI SIMBA ALIYEZUA TAHARUKI MKARANGO, msako wa Simba Mwingine Waendelea



Na Mwandishi Wetu, Lindi

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanikiwa kumdhibiti simba  mmoja dume aliyekuwa akihusishwa na matukio ya kushambulia mifugo na kuzua taharuki katika Kitongoji cha Songea, Kijiji cha Mkarango, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi leo Agosti 21, 2026, huku operesheni ya kumtafuta simba mwingine aliyekuwa pamoja naye ikiendelea.

Simba huyo amekamatwa majira ya saa 10 alfajiri na kikosi cha ufuatiliaji na udhibiti wa wanyamapori cha TAWA kutoka Kituo cha Selous Miguruwe baada ya kufuatilia mienendo ya simba hao kufuatia matukio ya kushambuliwa kwa mifugo yaliyoripotiwa katika Kijiji cha Mkarango.

Kwa mujibu wa taarifa ya kikosi hicho, katika nyakati tofauti simba hao walishamambulia na kuwajeruhi jumla ya ng'ombe 24 na kuua ng'ombe 17.

Kukamatwa kwa simba huyo ni sehemu ya jitihada zinazoendelea za TAWA katika kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao, kupunguza taharuki na kudhibiti changamoto zinazotokana na wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo mbalimbali nchini.

Simba huyo anatarajiwa kuhamishwa kutoka eneo hilo na kupelekwa katika eneo maalum la kutunzia wanyamapori hai mkoani Dar es Salaam.

Wakati huo huo, kikosi cha TAWA kinaendelea kufuatilia mienendo ya simba mwingine aliyekimbia wakati wa operesheni hiyo, huku juhudi zikielekezwa katika kuhakikisha anapatikana na kudhibitiwa.

TAWA inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha hali ya usalama na utulivu inadumishwa katika Kijiji cha Mkarango na maeneo mengine yanayokabiliwa na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu.

Post a Comment

0 Comments