Mbeto akikumbusha ACT kuheshimu matakwa ya katiba na sheria



Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi kimesema kuundwa kwa Kamati ya Pamoja ya utekelezaji wa  Ajenda za tamko la pamoja la maridhiano ni suala la kisiasa lakini ushiriki wa vyama vya Siasa katika Serikali  ya Umoja  wa Kitaifa Zanzibar (SUK) ni sharti la Kisheria na Kikatiba.

Kwa muktadha huo, CCM kimekitaka ACT  Wazalendo kuanza  kutekeleza  wajibu wa kushiriki serikalini wakati  mpango wa  kuundwa kwa Kamati ya pamoja ukiendelea kufanyika.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis,aliyesema Vyama vilivyokidhi matakwa ya sheria na kutakiwa kushiriki katika SUK ni faradhi. 

Mbeto  alisema CCM na ACT vina wajibu na shuruti ya kushiriki kwenye  serikalini kutokana na mahitaji ya Katiba huku  mchakato wa kuundwa kwa Kamati ya Pamoja ya Maridhaino, mchakato wake ukiendelea. 

Aliwataka Viongozi  wa ACT Wazalendo kutochanganya masuala hayo mawili kwa wakati mmoja, badala yake akawataka  watambue kuwa kila suala lina wakati na umuhimu wake.

"Kuundwa kwa Kamati ya Pamoja ya Maridhiano yenye Wajumbe toka CCMZ na ACT ni suala la Kisiasa.  Vyama hivyo vikumbuke ndivyo vyenye dhamana na wajibu wa kisheria na  kikatiba hivyo hivina hiari" Alisema Mbeto.

Aidha, alisema Vyama hivyo  vinapokuwa pamoja Serikalini ,ni rahisi kwao kukumbushana kuhusu utekelezaji wa hatua za kiutendaji za  Kamati  ya pamoja,kuliko chama kimoja kimo Serikalini na kingine kimetoroka.

"Sioni kama kuna tatizo. Kama lipo liko wapi hadi ACT kianze kusuasua. Kila kitu kiko wazi lakini  wenzetu wanataka kujenga taharuki  kwa wananchi ionekane kuna mjadala mkubwa bila kujali maslahi ya nchi" Alieleza 

Makubaliano na  hatua za utekelezaji wake ni mchakato usiohitaji shinikizo lolote,ndiyo maana hakuna muda mahsusi toka hatua moja hadi nyigine ,badala yake kila kitu kimewekwa kwa mpangilio na uwazi zaidi. 

"ACT  wasipoteze muda bure.Wasiwatie hofu wananchi kana kwamba kuna jambo kubwa mno losilowezekana.Kila kitu chini ya jua kinawezekana .Ndovu hajawahi kushindwa kubeba mkonga wake"Alisisitiza Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi alisema  pamoja na mbio zote za kisiasa,bado wananchi wanahitaji kupata  huduma muhimu na maisha bora yanayotokana na utendaji wa  shughuli za  kisera za serikali .

"Rais  wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi ndiye mwenye dhamana ya kuteua Kamati ya pamoja ya utekelezaji wa ajenda za Maridhiano. Tunamtaka Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Othman Masoud aache pupa na wahka. Zanzibar imepitia mengi na yote yamepita kwa  salama"Alikumbusha  Mbeto

Post a Comment

0 Comments