Na Magrethy Katengu,--DAR ES SALAAM
Tanzania imeungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Utambulisho, maarufu kama Identity Day, kupitia kampeni ya mwezi mzima itakayofanyika kuanzia Septemba 1 hadi 30, 2026, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kujisajili, kuchukua Vitambulisho vya Taifa na kuongeza matumizi ya utambulisho katika kupata huduma mbalimbali.
Kampeni hiyo inafanyika sambamba na maadhimisho ya Siku ya Utambulisho Duniani, ambayo huadhimishwa Septemba 16 kila mwaka. Nchini Tanzania, shughuli mbalimbali za maadhimisho hayo zitafanyika katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) zilizopo katika wilaya mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 1, 2026, jijini Dar es Salaam, Msemaji Mkuu wa Serikali, Grayson Msigwa, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya ya ID4Africa, taasisi inayojihusisha na kuhamasisha na kuimarisha mifumo ya utambulisho barani Afrika.
Amesema jumuiya hiyo imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wananchi wa Afrika wanapata utambulisho wa kisheria, ikiwa ni hatua muhimu katika kuwawezesha kupata huduma, haki na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
“Hadi kufikia Julai 2026, jumla ya watu zaidi ya milioni 27 walikuwa wamesajiliwa katika mfumo wa NIDA, ikiwa ni sawa na zaidi ya asilimia 87 ya watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea nchini,” amesema Msigwa.
Aidha, amesema zaidi ya Vitambulisho vya Taifa milioni 21 vilikuwa vimezalishwa, huku idadi kubwa ya wananchi tayari ikiwa imekabidhiwa vitambulisho hivyo.
Hata hivyo, bado kuna wananchi ambao wamekwishasajiliwa na vitambulisho vyao vimezalishwa, lakini hawajafika katika ofisi husika kuvichukua.
Maadhimisho ya Siku ya Utambulisho Duniani yanahusishwa na Lengo la 16.9 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), linalosisitiza umuhimu wa kuhakikisha watu wote wanapata utambulisho wa kisheria.
Utambulisho wa kisheria hauishii katika kuwa na nyaraka au kitambulisho pekee, bali ni msingi muhimu unaomwezesha mtu kutambulika kwa usahihi, kupata haki na huduma mbalimbali, pamoja na kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Katika kampeni hiyo, wananchi pia wameonywa dhidi ya kuwapatia watu wengine Vitambulisho vyao vya Taifa kwa ajili ya kusajili laini za simu au kufanya shughuli nyingine kwa majina yao.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakitoa vitambulisho vyao kwa ndugu, marafiki au watu wengine ili vitumike kusajili laini za simu, jambo ambalo linaweza kuwaingiza katika matatizo iwapo laini hizo zitatumika katika vitendo vya uhalifu.
NIDA imewataka wananchi kuhakikisha kuwa Kitambulisho cha Taifa kinatumika na mwenye kitambulisho mwenyewe na kutokitoa kwa mtu mwingine kwa matumizi yasiyo sahihi.
“Kitambulisho chako ni mali yako. Usimpe mtu mwingine akakitumie kusajili laini ya simu au kufanya shughuli nyingine kwa jina lako,” imeelezwa.
Mfumo wa utambulisho pia unaelezwa kuwa na umuhimu mkubwa katika kusaidia taasisi za ulinzi na usalama kudhibiti uhalifu wa kimtandao, utakatishaji wa fedha na vitendo vingine vya kihalifu kupitia uhakiki wa taarifa za watu.
Aidha, kaulimbiu ya kampeni ya Mwezi wa Utambulisho nchini ni “Kipo, Kichukue; Kamilisha Safari Yako,” ikiwa na lengo la kuwakumbusha wananchi waliojisajili na ambao Vitambulisho vyao vya Taifa vimekamilika kufika katika ofisi husika kuvichukua.

0 Comments