VIONGOZI WA KIMILA LONGIDO KUITISHA KIKAO KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NIÑO









NA ABRAHAM NTAMBARA, LONGIDO

Viongozi wa Kimila Wilaya ya Longido mkoani Arusha (Malaigwanani) wamepanga kufanya kikao maalum kwa ajili ya kupeana taarifa kuhusu uwepo wa mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa kuanza wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba hadi Desemba 2026, ili kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza katika maeneo yao.

Hayo yamebainishwa leo, Septemba 14, 2026, na Mwenyekiti wa Viongozi wa Kimila Wilaya ya Longido, Bw. Simon Melau, alipokuwa akizungumza katika kikao cha Kamati ya Maafa Wilaya ya Longido na Viongozi wa Tarafa ya Ketumbeine, kilicholenga kuwaelekeza viongozi hao kuwaandaa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua hizo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Agosti 18, 2026, iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), mvua kubwa za El Niño zinatarajiwa kuanza kuonekana kuanzia Septemba hadi Desemba 2026, huku uwezekano ukiwepo wa mvua hizo kuendelea hadi mwanzoni mwa mwaka 2027.

“Tupo tayari kusaidia Serikali yetu. Tutapokea maelekezo na kuyafanyia kazi. Mimi kama Mwenyekiti wa Malaigwanani, tutafanya kikao cha Malaigwanani Wilaya nzima na tutapita katika tarafa zote ili kuwapa taarifa hizi, kila mtu ajue kuna hatari kama hii na aweze kuchukua hatua. Lazima tufanye kazi na si kusubiri wakati huo ufike,” amesema Bw. Melau.

Ameutaka uongozi wa tarafa zote za Wilaya ya Longido kuanza mara moja kufanyia kazi maeneo yote hatarishi badala ya kusubiri mvua hizo zianze kunyesha ndipo waanze kuchukua hatua. Amesema viongozi wanapaswa kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi wanahamishwa mapema ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.

Aidha, ameiomba Serikali kufanya marekebisho katika maeneo ambayo miundombinu ya barabara imeharibika ili kujiandaa kukabiliana na athari za mvua hizo. Amesema baadhi ya maeneo yana makorongo ambayo yanaweza kuhatarisha maisha ya watu, huku mvua kubwa zikitarajiwa kusababisha baadhi ya barabara kutopitika na kufanya upatikanaji wa huduma muhimu, ikiwemo afya, kuwa mgumu.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Longido, Mhandisi Enock Raphael, amesema tayari wameandaa makadirio ya bajeti kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye changamoto.

Hata hivyo, amewataka viongozi kuwa na mawasiliano ya haraka pindi wanapobaini changamoto katika miundombinu ya barabara, ikiwa ni pamoja na kupiga picha na kuzituma kwa TARURA ili hatua za haraka zichukuliwe kurejesha mawasiliano.

 

 


Post a Comment

0 Comments