MSTAHIKI MEYA MANISPAA YA KIBAHA ARIDHISHWA NA KIWANDA CHA KEDS KUTENGENEZA MIFUMO YA MAJI MACHAFU




Na Victor Masangu,Kibaha

MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya  Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas amefanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda cha kutengenezea Pampasi kilichopo katika Kata ya Picha ya Ndege (KEDS) na kueleza kuridhishwa namna ambavyo kiwanda hicho kimetekeleza maagizo yake kwa kuweka mifumo mizuri ya mifereji katika kutiririsha maji machafu. 

Dkt.Nicas amefanya ziara hiyo  akiwa na timu ya wataalamu kutoka Manispaa ya Kibaha akiwemo afisa mazingira Bryson Mpogoza, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi Thobias Shilole,diwani wa Kata ya Picha ya Ndege Grace Jungulu.

Akiwa kiwandani hapo Dkt.Nicas amesema kuwa alipita kiwandani hapo miezi minne iliyopita na kukuta miundombinu mibovu ya utiririshaji maji machafu hali ambayo ilikuwa ikiathiri afya za Wananchi wanaoishi pembeni ya kiwanda hicho.

Amesema baada ya kuona hali hiyo Dkt.Nicas aliuagiza uongozi wa kiwanda hicho na kukipa siku saba kuhakikisha wanajenga miundombinu mizuri ya utiririshaji maji hayo ili kuhakikisha hayasambai kwa Wananchi.

Aidha amesema kwamba   ameamua kurudi kwa ajili ya kufuatilia kama maelekezo yake yamefanyiwa kazi na kwamba amefurahi kuona hali imekuwa nzuri kwakuwa wametekeleza maagizo na sasa hakuna malalamiko ya Wananchi juu ya kiwanda hicho kutiririsha maji machafu.

"Leo nimeamua kufanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda hiki kwa ajili ya kuja kuangalia kama maagizo yangu yametekelezwa lakini nimefurahi kuona uongozi wa kiwanda cha KEDS wamefanya yale tuliyokubaliana na hawa wanapaswa kupongezwa kwa kazi nzuri,"amesema Nicas

Aidha, Nicas amesema kuwa kiwanda cha KEDS ni kikubwa Tanzania kwani kimeajiri vijana wa Kitanzania zaidi ya 500 na kwamba ndio kiwanda pekee kikubwa kinachozalisha Pampasi hivyo Manispaa inakiheshimu kwa umuhimu wake.

Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanyakazi kubwa ya kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na bado Tanzania inawahitaji wawekezaji hivyo Manispaa ya Kibaha inafuata miongozo yote kama ambavyo Rais Samia ameelekeza.

Ameuomba uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha kinarudisha kwa jamii ambapo aliwaomba wasaidie ukarabati wa shule ya Msingi Lulanzi ambayo bati zake zimechakaa na kwamba wakati wa mvua madarasa yanajaa maji na kupelekea wanafunzi kushindwa kusoma.

"Niwaombe mtusaidie kukarabati shule yetu ya Msingi Lulanzi kwa kupaua bati mpya najua mnaweza kwani sasa hivi tunaelekea katika mvua za El-nino na wasiwasi wangu kwa hali jinsi ilivyo pale shuleni mvua ikishuka mambo yatakuwa magumu kwa wanafunzi na walimu ,"Amesema Nicas.

Kwa upande wake afisa biashara wa kiwanda hicho Derick Rwekaza, amesema kuwa baada ya kupewa maelekezo ya Meya juu ya kujenga mtaro huo walianza kazi maramoja na sasa hali ni nzuri kwakuwa hakuna malalamiko.

Rwekaza, amesema kuwa walichimba mtaro huo kwa zaidi ya urefu wa mita 600 kutoka kiwandani hapo na kwamba hatahivyo wataendelea kuchimba kwa zaidi ya mita 400 ili kuhakikisha Wananchi wote wanaondokana na kero juu ya maji machafu yanayotoka katika kiwanda hicho.

"Tumepata faraja baada ya kuona Meya wa Manispaa ya Kibaha ametupongeza kwa kutengeneza miundombinu mizuri ya mtaro wa kupitisha maji yanayotoka kiwandani hivyo nasisi tunasema tutaendelea kupanua mtaro huo kwa mita 400 nyingine ili kusudi Wananchi waishi katika mazingira mazuri,"amesema Rwekaza.

Kuhusu ombi la kusaidia shule ya Msingi Lulanzi Rwekaza amesema kuwa wamepokea ombi hilo na watalifanyiakazi kwa mujibu wa muongozo wa menejimenti ya kiwanda pamoja na ushirikiano baina ya Serikali ya Mtaa, Kata, diwani na Ofisi ya Meya wa Manispaa ya Kibaha.

Naye Meneja biashara wa KEDS Derick Deodatus amebainisha kwamba wameboresha mifumo ya mifereji kwa zaidi ya mita sita kwa lengo la kurahisisha maji hayo kuweza kupita kwa urahisi zaidi bila kukwama.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi Thobias Shilole amemshukuru Meya wa Manispaa ya Kibaha kwa jitihada zake kubwa za kufuatilia maendeleo ya Wananchi huku akimuomba aendelee kujitoa kwakuwa anachokifanya kimekuwa msaada mkubwa kwa jamii.

Baadhi ya Wananchi wanaoishi katika Mtaa huo akiwemo Ashura Amiri amepongeza hatua zilizochukuliwa na kiwanda cha KEDS kwa kuhakikisha wanachimba mtaro mkubwa wa kupitishia maji hayo kwani kwasasa adha na kero ya maji hayo imekwisha.

Post a Comment

0 Comments