Na mwandishi wetu,Mbeya
Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 zimezindua Mradi wa Darasa Janja katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Galijembe, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Uzinduzi wa mradi huo lengo lake kubwa ni katika kuboresha kwa kiasi kikubwa miundombinu ya elimu na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Mradi huu wenye lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufanisi wa ufundishaji kupitia teknolojia za kisasa, umegharimu jumla ya Shilingi milioni 79.207, kati ya hizo Shilingi milioni 59.55 zimetumika katika ujenzi wa darasa, Shilingi milioni 19.057 kwa ununuzi wa ubao janja (Smart Board).
Katika mradi huo nguvu za wananchi zimeweza kutumika katika uchimbaji wa msingi ikiwa na thamani ya kiasi cha Shilingi 600,000/-.
Ujenzi wa Darasa Janja ulianza tarehe 17 Novemba 2025 na kukamilika tarehe 22 Februari 2026 kwa asilimia 100. Shule ya Sekondari ya Wasichana Galijembe, ambayo ni shule ya bweni, ina jumla ya wanafunzi 522 na walimu 25.
Kadhalika darasa hilo linatarajiwa kuongeza fursa za wanafunzi na walimu kutumia teknolojia katika kujifunza, kufundisha, kufanya mikutano ya mtandao na kubadilishana uzoefu.
Kukamilika kwa mradi huu kunalenga kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika elimu na kuiwezesha shule kutoa elimu inayokidhi mahitaji ya karne ya 21. Uzinduzi wake na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 unaakisi juhudi za Serikali katika kuandaa mazingira bora ya elimu na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutumia teknolojia katika kujifunza na kujenga rasilimali watu yenye ujuzi kwa maendeleo ya Taifa.

0 Comments