Wanging’ombe, Njombe
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe imekamilisha ujenzi wa madaraja mawili, daraja la Wanging'ombe lenye urefu wa mita 30 katika barabara ya Wanging'ombe- Wangutwa pamoja na daraja la Ukomola lenye urefu wa mita 26.1 katika barabara ya Ukomola-Ipwani.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi hiyo, Meneja wa TARURA wilaya ya Wanging’ombe, Mhandisi Selemani Mziray amesema ujenzi wa madaraja hayo umetokana na changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa maeneo hayo ambapo kipindi cha mvua maji yalikuwa yakikata mawasiliano na kuzuia shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Amesema hali hiyo ilisababisha wananchi kushindwa kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine huku baadhi ya wanafunzi wakikosa fursa ya kufika shuleni kutokana na ugumu wa kuvuka maeneo hayo.
"Ujenzi wa madaraja haya mawili umetokana na kero kubwa iliyokuwa ikiwakabili wananchi hasa kipindi cha mvua walishindwa kutoka eneo moja kwenda jingine hali iliyosababisha hata watoto kushindwa kufika shuleni", amesema Mhandisi Mziray.
Aidha, Mhandisi Mziray ameeleza kuwa sambamba na ujenzi wa madaraja hayo, TARURA imeboresha mitaro ya kupitisha maji ili kuhakikisha maji yanapita katika njia zake bila kuathiri miundombinu ya barabara hususan katika kipindi hiki ambacho tahadhari ya mvua kubwa imetolewa.
Kwa upande wake, mkazi wa Wanging’ombe, Bw. Alex Benedict ameipongeza serikali kupitia TARURA kwa kukamilisha miradi hiyo akisema madaraja hayo yana umuhimu mkubwa katika kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo yanayohudumiwa na barabara hizo.
"Kipindi cha mvua tulishindwa kuvusha mazao na hata shughuli mbalimbali za kijamii zilisimama lakini kukamilika kwa miradi hii barabara zinapitika kipindi chote cha mwaka jambo litakalotusaidia kuendeleza shughuli zetu za kila siku", amesema Bw. Benedict.
Naye, Bw. Leonard Kayagala, mkazi wa Wanging’ombe amesema kukamilika kwa madaraja hayo kumetoa suluhisho kwa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi zikiwemo wanafunzi kushindwa kufika shuleni na wananchi kupata ugumu wa kufikia huduma muhimu za kijamii hususan huduma za afya.
Ameeleza kuwa miundombinu hiyo ni muhimu kwa kuwa inarahisisha usafiri na usafirishaji, inaongeza fursa za kiuchumi na kuwawezesha wananchi kupata huduma muhimu kwa wakati bila vikwazo.


0 Comments